0
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Mbeya imemhukumu kunyongwa hadi kufa polisi wa upelelezi, Maduhu, F 5842, aliyekuwa akikabiliwa na shitaka la mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU), Daniel Mwakyusa.

Aidha, mahakama hiyo imewaachia huru
washitakiwa wengine wawili wa kesi hiyo, polisi wa upelelezi, Shaaban, F 7769, na polisi wa kike mpelelezi, Neema, F 6545, baada ya kuwakuta
hawana hatia.

Hukumu hiyo ya kesi namba 16 ya mwaka 2013, ilitolewa jana mjini hapa na Jaji Rose Temba, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na
pande zote mbili.

Awali, ilielezwa mahakamani hapo na mawakili wa serikali, Archiles Mulisa akisaidiwa na Catherine Paul kuwa washitakiwa walifanya mauaji ya
kukusudia Februari 14 mwaka 2012 kinyume cha Kifungu Namba 196 cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa Marejeo mwaka 2002.

Mulisa alidai washitakiwa hao kwa pamoja walihusika na mauaji ya Daniel Mwakyusa baada ya kumpiga kwa kutumia silaha inayodhaniwa
kuwa ni bunduki, nje ya ukumbi wa starehe wa Universal uliopo Uyole jijini Mbeya.

Akitoa hukumu ya kesi hiyo, Jaji Temba alisema anawaachia huru mshitakiwa namba mbili, Shaaban ambaye alikuwa dereva wa gari ya polisi kwa kuwa ushahidi uliotolewa, unadhihirisha kuwa
alibaki ndani ya gari akimsubiri mshitakiwa namba moja aliyeshuka na kuingia kwenye ukumbi wa
Universal.

Kwa upande wa mshitakiwa namba tatu, Neema, Jaji Temba alisema aliridhishwa na mshitakiwa huyo kutohusika na mauaji kwa kuwa siku ya tukio alikuwa akijisikia vibaya, hivyo alilazimika
kubaki na dereva kwenye gari.

Jaji Temba alisema mshitakiwa namba moja, Maduhu, anahusika moja kwa moja na mauaji hayo, kutokana na ushahidi wa kimazingira, kwani
yeye ndiye aliyekuwa mtu wa mwisho kuondoka na Daniel Mwakyusa eneo la tukio na kumpeleka
kwenye gari.

Alisema sababu ya pili, ushahidi ulionesha kuwa silaha yake pekee ndiyo iliyotumika, tofauti na za askari wengine kwa kuwa risasi tatu zilionekana
kupungua kati ya zile alizokabidhiwa sambamba na ushahidi wa maganda matatu ya risasi, yaliyookotwa eneo la tukio.

Jaji Temba alisema sababu ya tatu ni kuwa ushahidi uliotolewa, unaonesha kuwa mshitakiwa huyo alikuwa wa mwisho kurejesha silaha, hivyo
kuhusishwa moja kwa moja na mauaji hayo.

Alisema kutokana na sababu hizo, mahakama inamtia hatiani kwa kuua kwa kukusudia, hivyo mshitakiwa Maduhu, amehukumiwa kunyongwa
hadi kufa.
Awali, ilidaiwa kuwa siku ya tukio ilikuwa Siku ya Wapendanao (Valentine’s Day), ambapo mtuhumiwa akiwa doria na askari wenzie, alimkuta Daniel Mwakyusa akiwa kwenye eneo la
starehe na mwanamke anayesadikiwa kuwa alikuwa pia na mahusiano na askari huyo.

Chapisha Maoni

 
Top