MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) hatimaye wametajamfanyabiashara ambaye alibainishwa na Rais John Magufuli katika hafla ya kuwaapisha Wakuu
wa Mikoa na Wilaya, Ikulu Dar es Salaam juzi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,
Valentino Mlowola alimtaja mfanyabiashara huyo
kuwa ni Mohammed Mustafa Yusuf Ali
anayetuhumiwa kuiibia Serikali matrilioni ya
shilingi kwa kutumia mashine za kielektroniki
(EFDs) ambazo hazijasajiliwa na TRA na kutoa risiti bandia.
Alisema TRA kwa kushirikiana na TAKUKURU
inaendelea na uchunguzi ili kubaini makampuni yote yanayojihusisha na udanganyifu huu,
ambapo hadi sasa jumla ya makampuni manne
yamebainika kujihusisha na ukwepaji kodi kwa mtindo huu kuanzia mwaka 2010 hadi 2014; na
jumla ya Sh 29,216,900,301.7 imebainika
kutokulipwa serikalini na makampuni hayo kwa kipindi hicho.
Alisema kwa sasa wanaendelea na mahojiano
naye zaidi ili kuwabaini wote wanaohusika na mfumo huo na kufikishwa katika vyombo vya
sheria.
Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa TRA, Alfayo kidata aliyeambatana na Mlowola katika mkutano
huo wa waandishi wa habari, makampuni hayo yamekuwa yakinunua risiti za manunuzi bandia
kutoka kwa watu wanaomiliki mashine za EFDs
ambazo hazijasajiliwa. “Makampuni hayo wakishanunua risiti za
manunuzi bandia, hatimaye huzitumia risiti hizo
kudai marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani
(VAT) bila kuwepo na bidhaa au huduma halisi
iliyouzwa au kutolewa na mhusika, kitendo
ambacho kinainyima serikali mapato stahiki kwa
mujibu wa sheria,” alisema.
Aliyataja makampuni hayo kuwa ni pamoja na
Skol Building Material Ltd ambayo tangu mwaka
2012 hadi 2013 haikulipa jumla ya VAT ya Sh
5,464,915,963 na Kodi ya Mapato yenye thamani
ya Sh 10,960,787,861 ambayo jumla ya kodi
inayodaiwa ni Sh 16,425,703,824 kwa kipindi
hicho.
Kampuni nyingine ni Farm Plant (T) Limited
ambayo tangu mwaka 2010 hadi 2014 haikulipa
jumla ya VAT ya Sh 5,930,170,573 na kodi ya
mapato yenye thamani ya Sh 4,948,393,516
ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni Sh
10,878,564,089.
Pia imo kampuni ya A.M.Steel & Iron Mills
Limited ambayo kuanzia mwaka 2013 hadi 2014
haikulipa jumla ya VAT ya Sh 79,016,112 na kodi
ya mapato yenye thamani ya Sh 131,693,518
ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni Sh
210,709,630.
Kampuni nyingine ni A.M Trailer Manufacturers
Limited ambayo tangu mwaka 2013 hadi 2014
haikulipa VAT ya Sh 638,221,034.80 na kodi ya
mapato yenye thamani ya Sh 1,063,701,724. 00
ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni Sh
1,701,922,758.00.
Alisema baada ya kubaini ukwepaji kodi huo kwa
kushirikiana na TAKUKURU inaendelea na
uchunguzi wa tuhuma hizo na mara baada ya
uchunguzi kukamilika hatua za kisheria
zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kukwepa
kodi.
Alitoa mwito kwa wafanyabiashara wote
kutojihusisha na kununua risiti za bandia na
kudai marejesho ya VAT yasiyostahili kwa kuwa
mamlaka imejizatiti kuendelea kuwabaini
wafanyabiashara wanaokwepa kodi na kuwafikisha
kwenye vyombo vya sheria kwa hatua stahiki.
Aidha alisema uchunguzi wa awali pia umebaini
kuwepo makampuni hewa 228 na kusisitiza
kwamba wameusimamisha mfumo huo bandia na
kutoa siku tatu kwa kampuni zote zinazodaiwa
kulipa fedha hizo.
“Hakuna yeyote anayekwepa kodi atasalimika,
wote ni lazima walipe na sasa tumedhibiti mfumo
huo bandia,” alisema.
Juzi Magufuli akizungumza na Ma RC na Ma DC
wapya, aliwataka wakasimamie vyema mapato
katika maeneo yao kwani kumekuwepo na baadhi
ya watu wajanja wanaotumia vibaya taasisi za
Serikali ikiwemo Wakala wa Usajili wa Kampuni
(Brela) TRA kujinufaisha wenyewe na kuliingizia
taifa hasara.
Alisema: “Tulikuwa tunafuatilia mashine za EFDs
zinazokusanya mapato, yupo mtu mmoja
alitengeneza kampuni nyingi zilizokuwa zikimlipa
asilimia tano ya VAT na yeye anacheza na TRA
halipi asilimia 18 ya kodi hiyo. Alikuwa anaingiza
kati ya shilingi milioni saba mpaka nane kwa
dakika. Serikali ilipoteza matrilioni ya fedha. Huyu
mtu yupo kwenye mikono salama kwa sasa”.
Chapisha Maoni