Mkataba wa Msuva unamalizika mwakani ila kiwango chake kizuri kimepelekea apendekezwe kupata mkataba mpya
Mabingwa wa soka Tanzania Bara Klabu ya Yanga , wameanza kutekeleza maadhimio yao ya kutopoteza nyota yake yeyote kwenye kipindi hiki cha usajili baada ya kutenga Sh. Milioni 60, kwa ajili ya kumwongeza mkataba mpya winga wao tegemeo Simon Msuva.
Mkataba wa Msuva, unamalizika mwakani na kocha, uongozi wa timu hiyo kwa kushirikiana na kocha mkuu George Lwandamina, umependekeza aongezewe mkataba kutokana na mchango wake ndani ya timu.
Charles Boniface Mkwasa, ameiambia
Goal, wameamua kuanza na Msuva kwasababu walishaanza kuongea naye kuhusu kuongeza mkataba mpya na wanatarajia kukamilisha zoezi hilo mara mchezaji huyo atakapomaliza majukumu ya timu ya taifa ‘Taifa Stars’.
“Mikakati yetu ni kuhakikisha hatupotezi mchezaji yeyote ambaye amekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi chetu cha msimu ujao na sasa tumeanza na Msuva, baada ya kumalizana naye tutahamia kwa wengine hadi kuhakikisha wote wanamalizika,”amesema Mkwasa.
Katibu huyo alisema wanafanya hivyo siyo kuwahofia wapinzani wao Simba, ambao wamekuwa wakitamba kumsajili mchezaji huyo bali ni mikakati ambayo wamejiwekea na hiyo inatokana na utashi na mapenzi aliyokuwa nayo mchezaji mwenyewe.
Aidha Mkwasa amesema hadi sasa hawajapokea barua yoyote kutoka kwa klabu ya ndani au nje ya nchi ikieleza kumuhitaji Msuva kwa ajili hata ya majaribio na kudai kwamba endapo itatokea wataikaribisha kufanya nao mazungumzo na wakielewana wanamruhusu mchezaji huyo.
Mahasimu wa Yanga, klabu ya Simba wamekuwa wakimwania Msuva, kwa udi na uvumba, lakini hivikaribuni wamekiri kuwa ni vigumu kumpata mchezaji huyo mwenye kasi ya ajabu awapo uwanjani kutokana na klabu yake kumtegemea zaidi , mbali na timu hizo pia Mabingwa maratano wa Afrika Zamalek wanatajwa kuwania saini yake.
Chapisha Maoni