0
Chelsea wamepiga hatua sana katika mazungumzo yao ya kutaka kumnunua mlinda lango Kepa Arrizabalaga kutoka klabu ya Athletic Bilbao ya Uhispania katika uhamisho ambao utavunja rekodi ya nunua ya ununuzi wa golikipa.
Mlinda lango huyo mwenye miaka 23 anatarajiwa kununuliwa kujaza nafasi ya Thibaut Courtois ambaye anaonekana kutokuwa tayari kusalia katika klabu hiyo ya Stamford Bridge.
Ada hiyo itazidi £66.8m ambazo Liverpool walilipa mwezi Julai kumchukua kipa wa Brazil Alisson.
Courtois, ambaye huchezea timu ya taifa ya Ubelgiji, bado hajarejea mazoezini huku tetesi zikimhusisha na kuhamia Real Madrid.

Mchezaji huyo mwenye miaka 26 alikuwa ametarajiwa kujiunga na wenzake kwa mazoezi ya kuanza msimu Jumatatu lakini hakufika.
Inadaiwa anataka kulazimisha uhamisho wake kwa kuwa klabu yake haikuwa inataka kumuuza.
Alipoulizwa kuhusu Kepa baada ya Chelsea kuwashinda Lyon wa Ufaransa kwa mikwaju ya penalti Jumanne, meneja wa Chelsea Maurizio Sarri alisema: "Nilimwona mwaka mmoja uliopita. Maoni yangu ya kwanza yalikuwa kwamba yeye ni kipa mzuri sana, wa umri mdogo, lakini mzuri sana."
Iwapo ununuzi wa Kepa utafanikiwa, basi itakuwa ni rekodi pia kwa klabu hiyo ya London katika ununuzi wa wachezaji.

Bei yake itazidi £58m walizowalipa Real Madrid kumchukua mshambuliaji Mhispania Alvaro Morata mwaka jana.
Kepa ni kipa nambari mbili katika timu ya taifa ya Uhispania, akiwa nyuma ya kipa wa Manchester United David de Gea, na amechezea timu ya taifa mechi moja pekee.
Amekaa misimu miwili katika kikosi cha kwanza cha Bilbao na kuwalindia lango katika mechi 53 La Liga.


Kwamujibu wa 
BBC SWAHILI

Chapisha Maoni

 
Top