Manchester United watakabiliwa na "msimu mgumu" iwapo hawataimarisha kikosi chao kwa kuwanunue wachezaji wapya kabla ya kipindi cha kuhama wachezaji kufungwa Alhamisi.
Hiyo ndiyo tahadhari iliyotolewa na meneja wao Jose Mourinho.
Hii ni baada ya Mashetani Wekundu kukamilisha mechi za kirafiki za kujiandaa kwa msimu mpya kwa kuchapwa 1-0 na mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich siku ya Jumapili.
Javi Martinez alifunga kwa kichwa bao pekee katika mechi hiyo ambayo Bayern waliitawala.
"Afisa Mkuu Mtendaji wangu (wa Man Utd) anafahamu ninataka nini na bado nina siku kadha za kusubiri na kuona nini kitatokea," Mourinho alisema akizungumza na runinga ya klabu hiyo MUTV.
"Klabu hizo nyingine zinazoshindana nasi zina nguvu sana, zimejiimarisha sana na tayari zina vikosi vizuri sana. Au wanawekeza sana kwa mfano Liverpool, ambao wananunua kila kitu na kila mtu.
"Tusipoboresha kikosi chetu basi utakuwa msimu mgumu sana kwetu."
United kufikia sasa wamewanunua wachezaji watatu tu kipindi cha sasa cha kuhama wachezaji.
Wachezaji hao ni kiungo wa kati Mbrazil Fred aliyewagharimu £47m, beki Mreno Diogo Dalot na kipa nambari tatu Lee Grant.
Wataanza kampeni yao Ligi ya Premia kwa mechi dhidi ya Leicester City uwanjani Old Trafford Ijumaa.
Afisa mkuu mtendaji wa zamani wa United Peter Kenyon alisema Jumapili kwamba Mourinho anafaa kutafuta njia ya "kutatua" mzozo wake na naibu mwenyekiti mtendaji wa United Ed Woodward.
United butu katika mashambulizi
United walikamilisha maandalizi ya msimu mpya kwa njia isiyo ya kuridhisha, ambapo walikuwa butu katika mashambulizi yao kwenye lango lililokuwa linalindwa na Manuel Neuer.
Kasi ya Marcus Rashford iliwapa matumaini United lakini alikuwa hapati mpira sana kwa kipindi kirefu kwenye mechi hiyo.
Kiungo wa kati aliyeshinda Kombe la Dunia na Ufaransa Paul Pogba, mshambuliaji wa Ubelgiji Romelu Lukaku na mshambuliaji wa England Jesse Lingard walikuwa miongoni mwa wachezaji ambao hawakuwemo kwenye kikosi cha United kilichocheza mechi hizo za kirafiki.
Kurejea kwao kutaimarisha safu yao ya mashambulizi ingawa Mourinho bado hajatulia.
Kuna utata kuhusu mustakabali wa Anthony Martial, na pia kuna wachezaji wengine wa klabu hiyo ambao hawajashiriki maandalizi ya msimu mpya na wanatarajiwa kuhama.
Kufikia sasa haiko wazi United watakuwa katika hali gani watakapokutana na Leicester.
Tamko la Mourinho kabla ya kuanza mechi linaashiria kwamba bado anataka kuwanunua wachezaji wengine.
Beki wake Eric Bailly aliondoka uwanjani kipindi cha pili baada ya kugongana na Serge Gnabry.
Mourinho anataka sana kuimarisha sehemu ya kati kwenye safu ya ulinzi lakini kutokana na uchezaji wa Jumapili, huenda akalazimika pia kufikiria kuhusu safu ya mashambulizi.
Kwamujibu wa
BBC
Chapisha Maoni
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.