0
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wilayani Mbogwe mkoani Geita Omari Atanas, amekamatwa na maofisa Uhamiaji wilayani hapa kurudishwa kwao nchini
Rwanda baada ya kubainika sio raia wa Tanzania.

Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Mkuu wa wilaya hiyo, Aman Mwenegoha, alisema Mwenyekiti huyo alikamatwa Desemba 22, mwaka huu na maofisa
Uhamiaji na kuhojiwa kwa muda na kugundulika sio raia wa Tanzania bali ni raia wa Rwanda.

Mwenegoha alisema , awali tetesi za uraia wa Atanas, zilianza wakati wa kampeni za Uchaguzi wa Serikali wa Mitaa uliofanyika hivi karibuni
nchini, baada ya Mwenyekiti huyo kufika kijiji cha Luganga.

Baada ya kufika kijijini hapo ambapo inadaiwa kuna Wanyarwanda wengi aliwahamasisha kufanya vurugu kwa kuwa serikali haitaki kuwapa vibali
vya uraia.

Mwenegoha alisema baada ya mahojiano ya siku tatu, ndipo ilibainika kuwa mwenyekiti huyo sio raia wa Tanzania bali wa Rwanda na walimsafirisha hadi Rwanda, ambako alitambuliwa ni raia wa nchi hiyo na ana mke na watoto wawili.

“Baada ya kumfikisha Rwanda wale maofisa walimhoji na baadaye kumtambua kuwa ni raia wa
nchi hiyo na wakati anakuja Tanzania walimpa kitambulisho, zaidi ya miaka 15, iliyopita na wakamgundua kuwa anayo familia ya mke na watoto wawili”, alisema Mwenegoha.

Kwa upande wake, Atanas alisema alifika nchini mwaka 2000 na kuishi katika Kitongoji cha Manzese kata ya Busoka wilayani Kahama, ambapo mwaka 2003 alihamia kijiji cha Luganga
wilayani Mbogwe na kuishi hapo hadi
alipokamatwa mwanzoni mwa wiki hii.

Kuhusu wahamiaji waliopo katika wilaya hiyo, Mwenegoha alisema wahamiaji 14, ndio walioomba uraia wa Tanzania na kupewa baada ya kukana uraia wa nchi zao na kwamba katika orodha hiyo yeye hayumo.

Hata hivyo Atanas anadaiwa baada ya kukamatwa na kurudishwa kwao ameacha deni la Sh milioni
1.5 alizokopa kutoka kwa Katibu Mwenezi wa Chadema (hivi sasa kahamia CCM) kwa ajili ya kufanya kampeni katika uchaguzi wa Serikali za
Mitaa.

 Mwenegoha alisema pamoja na yote
kunaonekana kuna uzembe mkubwa uliofanywa na uhamiaji wilayani humo kwa kushindwa kumbaini mapema kiongozi huyo ambapo alisema
atakaa na kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo ili kujadili suala hilo.

Hata hivyo Mwenegoha alisema kwa sasa eanajipanga kufanya operesheni kubwa ya kuwasaka wahamiaji wote haramu ili sheria ichukue mkondo wake ikiwemo kuwarudisha kwao
watakaobainika.

 Kwa upande wao Chadema walipoulizwa kuhusu tukio hilo walisema hawana taarifa na kwamba watafuatilia kufahamu undani wake.

Akizungumza na mwandishi jana, Msemaji wa Chama hicho, Tumaini Makene alisema, “Ndio kwanza unatupa taarifa hatufahamu tukio hilo, ila
tutafuatilia”, alisema Makene.

Chapisha Maoni

 
Top