0

Uongozi wa Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam
umesema kuwa haupo tayari kumfuatilia mchezaji
ambaye hana mapenzi ya kuichezea timu hiyo.
Kauli hiyo ya Simba imekuja siku moja baada ya
taarifa kuwa mshambuliaji aliyekuwa anasubiliwa
na uongozi wa timu hiyo, Laudit Mavugo wa Vital
'O ya Burundi kudaiwa kutimkia Ufaransa kufanya
majaribio ya kucheza soka la kulipwa kwenye
klabu ya Tours FC.
Katika mahojiano maalum na Nipashe, Katibu
Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele alisema kuwa
wameshangazwana taarifa hizo za Mavugo
kutimkia Ufaransa wakati tayari walikuwa na
makubaliano ya kuja nchini kuanza kuitumikia
timu yao.
Kahemele alisema kuwa wanafikiria kuachana na
Mavugo kwa sababu ameonekana kutokuwa na
mapenzi ya dhati ya kuja kuitumikia Simba kama
walivyokubaliana hapo awali.
"Mara ya mwisho tulipowasiliana naye alikuwa
anasubiri amalize mechi za timu yake ili aje
kujiunga na sisi, na makubaliano yetu alikuwa
anakuja kujiunga moja kwa moja bila kufanya
majaribio, kama ameamua tofauti hatuna haja ya
kumlazimisha," alisema Kahemele.
Alisema kuwa bila ya Mavugo, Simba inatarajia
kufanya vizuri katika msimu jao kutokana na
wachezaji waliowapata pamoja na mabadiliko
waliyofanya kwenye benchi la ufundi.
"Afrika kuna wachezaji wengi, na hatuwezi kufanya
kazi na mtu ambaye ni hana moyo wa kuitumikia
klabu yetu, sisi tunaendelea kupokea wachezaji
wengine ambao wanakuja kufanya majaribio na
walio tayari kuitumikia Simba," Kahemele alisema.
Aliongeza kuwa jana usiku walitarajia kupokea
wachezaji wawili wapya kutoka Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambao leo
wataelekea Morogoro kuungana na kikosi cha timu
hiyo kwa ajili ya kufanya majaribio
yanayosimamiwa na Kocha Mkuu Joseph Omog.
Aliwataja wachezaji hao waliotarajiwa kuwasili
nchini jana kuwa ni kiungo kutoka FC Lupopo ya
Kongo na Masanga Masoud Fredrick ambaye ni
mshambuliaji.



Posted Africa News Sports

Chapisha Maoni

 
Top