0
Jeshi la polisi nchini linawashikilia vijana 36 wa kundi maarufu Panya Road wanaodaiwa kufanya vurugu na kupora mali za watu na kusababisha taharuki katika jiji la Dar es salaam huku baadhi
ya wananchi wakitoa maoni tofauti kuhusiana na tukio hilo.

Akitoa ufafanuzi wa taharuki hiyo msemaji wa jeshi la polisi SSP ADVERA BULIMBA ambaye mbali na kuwatoa hofu wananchi kuwa hali hiyo haitajitokeza tena amesema jeshi hilo limejipanga vizuri kukabiliana na vikundi vyovyote vinavyotaka kuvuruga amani ya nchi.

Pia amesema kwamba endapo polisi
wasingewadhibiti vijana hao mapema tangu wakiwa makaburini baada ya kumzika mwenzao aliyeuawa na wananchi baada ya kuiba hali
ingekuwa mbaya zadi.

Kufuatia tukio hilo baadhi ya wananchi wa maeneo ya Magomeni ambako vurugu zilianzia wameelezea namna zilivyoanza hadi kusababisha
watu kuanza kukimbia hovyo na wengine kuacha maduka yao wazi na taarifa kusambaa maeneo
mengine.

Katika maeneo ya Mwananyamala na Ubungo baadhi ya waliozungumzia sakata hilo wameitaka serikali kuangalia makundi ya vijana na ikiwezekana wapatiwe elimu ya ujasiriamali bure
ili waweze kuendesha maisha.

Wananchi wengine wameshauri vijana wasiokuwa na kazi mitaani wapelekwe jeshini wakafundishwe stadi za kazi pamoja na uzalendo ili kuepuka
vitendo hivyo.

Taharuki hiyo ilitokea usiku wa tarehe 2 Januari, 2014 chanzo kikiwa ni kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la MOHAMED AYUB kuuawa na wananchi
tarehe mosi mwaka huu katika maeneo ya Tandale kwa Mtogole kwa tuhuma za wizi ambapo tarehe 2 maziko yalifanyika na taarifa zilizolifikia jeshi la polisi zilidai kuwa baada ya maziko vijana wenzake walijipanga kufanya fujo ili kulipiza
kisasi.

Chapisha Maoni

 
Top