0
Baada ya kutangaza vita dhidi ya mashoga juzi,
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
jana alitangaza vita nyingine; hataki uvutaji
shisha akisema inachanganywa na vilevi
vinavyoharibu vijana.
Makonda, ambaye alikuwa akihutubia Tamasha la
Vijana lililoandaliwa na Upendo Media Group
kwenye Uwanja wa Taifa aliagiza wavuta shisha
hadharani, sigara na mashoga wakamatwe ndani
ya siku saba.
“Ni marufuku biashara ya shisha kwenye mkoa
wangu. Wanaofanya bishara hiyo wote
nitawakamata. Mimi ndiye mbabe wa vita,”
alisema Makonda na kuongeza: “Nina imani
watakuwa wamefungasha virago vyao iwe ni
kwenye klabu au baa maana humo
wanachanganya vitu vingi; bangi na vilevi
ambavyo vina madhara.”
Alisema vijana wa vyuo na sekondari ndiyo
waathirika wakubwa wa kilevi hicho, ambacho
huvutwa kwa njia ya bomba la mpira linalotoka
kwenye jiko maalumu ambalo tumbaku
huunguzwa na kutoa moshi.
“Baada ya siku saba tutakutana (Gereza la
Segerea),” alisema.
“Kwa utafiti nilioufanya chini ya TFDA, shisha ina
madhara makubwa kwa wanaoivuta na wasiovuta.
Inasababisha kansa ya mapafu na koo.
“Na pia inasababisha utegemezi ambapo mtu bila
kuvuta hawezi kuona maisha, lakini pia
inapunguza uwezo wa kufikiri na inamaliza nguvu
kazi katika taifa,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO),
kiwango cha shisha inayovutwa kwa saa moja, ni
sawa na kuvuta sigara kati ya 100 na 200.
Utafiti wa shirika hilo unaonyesha kuwa mvuta
sigara wa kawaida huingiza nusu lita ya moshi
kwa kila sigara, lakini mvuta shisha ni zaidi ya
hivyo.
Kuhusu uvutaji wa sigara, Makonda alisema ndani
ya siku saba zijazo ni marufuku kuvuta sigara
hadharani na kila anayehitaji kufanya hivyo
atapaswa kutafuta sehemu iliyojitenga ili akate kiu
yake.
“Kila anayevuta sigara, atapaswa kuvuta sehemu
ambayo hatawabughudhi wenzake.
"Tumechoka kupanda magari na watu wanaovuta
sigara, kukaa hoteli na watu wa aina hiyo. Sasa
mvutaji anapaswa kuvuta sehemu ya peke yake,
na sio kwenye jumuiko la watu. Madhara ni
makubwa kwa tusiovuta kuliko wanaovuta, ”
alisema.
Maagizo ya Makonda yanakuja ikiwa ni wiki moja
tangu apige marufuku abiria na dereva wa
bodaboda kusafiria chombo hicho bila ya kuvaa
kofia ngumu.
Alisema kupanda pikipiki bila kofia hiyo ni
dhamira ya kutaka kujiua kwa sababu dereva na
abiria wakipata ajali ni rahisi zaidi kupoteza
maisha iwapo kichwa kitajipiga ardhini.
“Nimewasiliana na kamati yangu ya usalama
barabarani ya mkoa. Hili nitalisimamia kikamilifu
lazima wote wavae helmet na wakikamatwa wote
watashtakiwa,” alisema.
Mapema mwaka huu, mara baada ya kuteuliwa
kuwa Mkuu wa Mkoa, Makonda alitoa maagizo
matatu yanayohusu ombaomba wa barabarani
kuondoka na kubomolewa kwa majengo makubwa
yaliyojengwa kinyume na taratibu na yasiyo na
maegesho.
Agizo la tatu la Makonda lilikuwa ni wamiliki wa
baa kutopiga muziki nje ya utaratibu wa vibali
vyao.
Makonda pia alirudia wito wake wa kutaka watu
wanaojishughulisha na biashara ya ushoga
wakamatwe mara moja.
Alisema miaka michache iliyopita Taifa lilikataa
msaada wenye sharti la ushoga, lakini
inashangaza kuwa bado zipo taasisi zisizo za
kiserikali zilizoundwa kwa ajili ya kutoa misaada
kwa watu wanaojihusisha na vitendo hivyo.
“ Nimefanya mazungumzo na Waziri wa Katiba
na Sheria. Hatutaki hili liendelee kwa sababu hiyo
naiagiza TCRA kuwa wapo watu wanaojitangaza
kwenye instagram na vyombo vya habari kwamba
wao ni mashoga, wakamatwe haraka
iwezekanavyo na kama kuna shoga ana akaunti
kwenye mitandao ya kijamii na wale wafuasi wake
wote ni watuhumiwa sawasawa na mhusika,”
alisema.
Ushoga, ambao ni uhusiano wa mapenzi wa watu
wa jinsia moja, ni marufuku nchini, kwa mujibu
wa Sheria ya Adhabu.
Kwa mujibu wa Sura ya 16, sehemu ya 154, mtu
anayejihusisha na ngono na mtu mwingine
kinyume na maumbile au anayemruhusu mtu
mwingine kufanya naye ngono kinyume na
maumbile, atakuwa amefanya kosa la jinai na
kustahili kifungo cha miaka 14 jela.





chz
Mpekuzi

Chapisha Maoni

 
Top