Kada aliyeteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya
Mbozi, Ally Muswanya ameachia wadhifa huo hata
kabla ya kuapishwa.
Wakati uteuzi wa makada watatu wa kwanza
ulisahihishwa na Ikulu, Maswanya hajaibuka
kwenye hafla ya kiapo na tayari mtu mwingine
amekwenda kuziba nafasi yake.
Maswanya, ambaye alikuwa aapishwe juzi na
mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa,
hakuapishwa na badala yake aliapishwa John
Palingo ambaye katika uteuzi uliotangazwa na
Ikulu alikuwa aongoze Wilaya ya Kongwa.
Taarifa za Maswanya kuachia nafasi hiyo zilianza
kusambaa kwenye mitandao ya kijamii juzi usiku
zikieleza kuwa amejiuzulu nafasi hiyo, lakini
haikuelezwa sababu za kuchukua uamuzi huo wa
kukataa kumwakilisha Rais wilayani.
Hata hivyo, Maswanya, ambaye ni meneja wa
kampuni ya huduma za simu ya Tigo, Kanda ya
Ziwa, hakutaka kuzungumzia kwa kina sakata
hilo.
“Kama ambavyo inajulikana, mimi ni meneja wa
Kanda wa Tigo,” alisema Maswanya
alipozungumza na Mwandishi
“Hayo ndiyo yako kwenye mamlaka yangu
kuzungumzia. Kama ni suala la Tigo, karibu
tuzungumze yote kuhusu mipango na mikakati
yetu.”
Maswanya alisema kwa sasa, nguvu akili na
uwezo wake wote anaelekeza katika kutimiza
wajibu kwenye nafasi hiyo yake Kanda ya Ziwa.
Hata baada ya kuulizwa kama ndiye aliyekataa
uteuzi, Maswanya alisisitiza “Hayo
yatazungumziwa na mamlaka husika ambazo
naamini kwa nafasi yako unazijua.”
Alipoulizwa kama Maswanya alihudhuria hafla ya
kula kiapo ya wakuu wa wilaya katikati ya wiki,
kaimu mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano ya
Rais, Gerson Msigwa alisema hafahamu kama
alikuwapo au la kwa kuwa wengi ni wakuu wapya
hivyo haikuwa rahisi kwake kujua nani hakuwapo.
Sarakasi ya meneja huyo kutochukua madaraka
aliyopewa na Rais inafanya idadi ya watu
walioteuliwa na kushindwa kuanza kazi kutokana
na sababu tofauti kufikia wanne.
Kabla ya wakuu wateule kula kiapo cha maadili
Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alieleza
kuwa uteuzi wa wakuu hao ulifanywa kwa makini
na kwamba anafahamu kwa majina watu wote
aliowateua, akisema alizingatia umri, elimu na
uzoefu.
Tukio la kwanza lilikuwa la uteuzi wa Fikiri Said
kuwa mkuu wa Wilaya ya Ikungi, lakini
akabadilishwa kwa maelezo kuwa jina lake
liliwekwa kimakosa. Badala yake aliyekuwa katibu
wa CCM wa Mkoa wa Mwanza, Miraji Mtaturu
akateuliwa kuchukua nafasi hiyo.
Pia aliyeteuliwa kuongoza Wilaya ya Rombo,
Fatma Toufiq alibadilishwa kwa maelezo kuwa
tayari alishakuwa na wadhifa mwingine wa
ubunge wa viti maalum na nafasi yake akapewa
Agness Hokororo.
Rais John Magufuli alisema wakati akielezea suala
hilo kuwa hakutaka mtu ashike nafasi mbili kwa
wakati mmoja na kwamba hiyo ndiyo tafsiri ya
falsafa ya “Hapa Kazi Tu”.
Tukio lililokuwa la aina yake katika uteuzi huo ni
la kubatilisha uteuzi wa Emile Ntakamulenga
aliyetangazwa kuwa mkuu wa Wilaya ya
Serengeti.
Hakukuwa na taarifa za awali za kubatilisha
uteuzi huo na Ntakamulenga alienda Ikulu kama
makada wengine, akaruhusiwa kujisajili na
kuingia kwenye viwanja vya makazi hayo makuu
ya nchi.
Lakini wakati akisubiri kula kiapo cha maadili, Jaji
Salome Kaganda akatoa maelezo kuwa kulifanyika
makosa katika kutangaza jina lake na kwamba
aliyekusudiwa alikuwa Nurdin Babu ambaye naye
alikuwa ameitwa Ikulu siku hiyo.
Kutokana na makosa hayo, Jaji Kaganda alisema:
“Naomba utupishe” na ndipo Ntakamulenga
akanyanyuka na kuanza kuondoka kutoka viunga
vya Ikulu akiacha maswali.
Akizungumzia kutoapishwa kwa Maswanya kuwa
mkuu wa Wilaya ya Mbozi na badala yake
kumwapisha Palingo, Mkuu wa Mkoa wa Songwe,
Chiku Galawa alisema alipokea ujumbe mfupi kwa
njia ya simu kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi
akijulishwa kwamba mtu aliyekuwa amepangiwa
wilaya hiyo, John Ernest Palingo amebadilishwa
kituo cha kazi, hivyo ataongoza Mbozi.
Galawa alisema alipokea maelekezo ya ujumbe
huo kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi kwamba
ampokee na kumuapisha ili aanze kazi mara
moja, lakini akaongeza kuwa hana taarifa za mtu
aliyeteuliwa awali kuwa bosi wa Mbozi.
“Nilichofanya ni kutekeleza maagizo ya mkuu
wangu,” alisema Galawa.
“Pia mimi nilichokuwa nahitaji ni kukamilishiwa
ma-DC wangu kwa wilaya zote, hivyo jana (juzi)
asubuhi nilifanya mawasiliano na DC
aliyeelekezwa na Katibu Mkuu Kiongozi,
tukamtumia tiketi ya ndege na jana (juzi) mchana
alifika na nikamuapisha kwa kuwa ni DC wa
Mbozi pekee aliyekuwa amebaki.”
Alisema siku ya Alhamisi alimuapisha mkuu wa
Wilaya ya Ileje, na kwamba wengine wa wilaya za
Momba na Songwe hawakutumiwa tiketi mapema,
lakini walifika na juzi asubuhi aliwaapisha wakati
wakimsubiri Palingo.
Alisema kazi ya kwanza kuwapangia ni mbio za
Mwenge wa Uhuru ambao uliingia jana asubuhi
mkoani kwake ukitokea Mbeya. Alisema mwenge
huo utawawezesha kufahamu vyema jiografia ya
wilaya zao.
Mkoani Dodoma, Jordan Rugimbana aliwaapisha
wakuu wapya sita kati ya saba wa wilaya za mkoa
huo baada ya Rais Magufuli kufanya mabadiliko
madogo.
Baada ya kuwaapisha wakuu hao wa wilaya,
Rugimbana alielezea mabadiliko hayo ya Rais
yaliyofanya akosekane mteule wa wilaya moja.
“Aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa
sasa atakwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi
baada ya aliyeteuliwa kujiuzulu,” alisema.
Alisema kutokana na mabadiliko hayo, Wilaya ya
Kongwa inasubiri uteuzi mwingine utakaofanyika
wakati wowote kuanzia sasa.
Wakuu wa wilaya walioapishwa Dodoma ni
Elizabeth Kitundu (Bahi), Vumilia Nyamoga
(Chamwino), Simon Odunga (Chemba), Christina
Mdeme (Dodoma Mjini), Veneranda Makota
(Kondoa) na Jabir Shekimweri (Mpwapwa).
Posted Africa Newss
Chapisha Maoni