binafsi juu ya nafuu ya kodi ya mishahara, huenda
likaondoka baada ya takribani benki zote nchini
kutangaza ongezeko la asilimia 18 kwenye
huduma za kuhifadhi na kutoa fedha.
Wachumi mbalimbali walisema jana kuwa mbali na
wafanyakazi, ambao wataathirika na ongezeko hilo
kwa sababu mishahara yao inapitia benki, pia watu
wote wanaotumia benki, wakiwamo
wafanyabiashara, wanafunzi na wengine wote
wanaotumia huduma za kibenki, wataumia pia kwa
kukatwa fedha zaidi wanapofanya miamala ya
kibenki.
Walisema hali hiyo inaweza kufanya watu waamue
kukaa na hela majumbani mwao, kitendo ambacho
kitaongeza matukio ya uhalifu kwa majambazi
kuvamia majumbani.
Ongezeko hilo limetokana na marekebisho ya
Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT),
Sura 148, yaliyotangazwa na Waziri wa Fedha na
Mipango, Dk Philip Mpango, alipokuwa akisoma
bajeti ya serikali bungeni kwa mwaka wa fedha
2016/17.
Alisema serikali inakusudia kutoza kodi ya
ongezeko la thamani kwenye ada za huduma za
kibenki zinazotozwa na benki zote nchini ili
kupanua wigo wa kodi.
Kufuatia hali hiyo, takribani benki zote nchini
zilitangaza ongezeko hilo la kodi walilosema
linatokana na bajeti mpya ya serikali ya mwaka wa
fedha 2016/17, ambayo utekelezaji wake unaanza
leo.
Katika tangazo la benki ya NMB jana, ilielezwa
kuwa gharama zote za miamala na huduma za
kibenki katika machapisho yaliyotolewa hapo awali
zitakuwa na ongezeko la asilimia 18 ya VAT
kuanzia Julai Mosi (leo).”
Pia matangazo ya benki za Standard Charterd,
Akiba Commercial Bank (ACB) na CBA yalikuwa na
maelezo kama lile la NMB, ingawa lenyewe lilieleza
zaidi kuwa kodi hiyo haitahusu riba za mikopo.
Makato hayo yatagusa watu wengi kwani
mishahara ya watumishi wa umma na ile ya
wafanyakazi walioajiriwa kwenye sekta binafsi
hulipwa kupitia benki mbalimbali nchini.
MAKATO MAPYA
Kwa upande wa ada ya akaunti ya benki kwa
mwezi, baadhi ya taasisi hizo za kifedha humtoza
kila mteja kati ya Sh. 1,500 mpaka Sh Sh. 2,000
kwa mwezi.
Kwenye upande wa miamala inayofanyika kupitia
mashine za kutolea fedha (ATM), benki hutoza
wastani wa Sh. 800 hadi Sh. 1,500 kutegemea na
aina ya kadi ambayo mteja anaitumia.
Baada ya ongezeko la asilimia 18 ya VAT kwenye
tozo za benki, gharama za kuhifadhi akaunti za
mteja kwa mwezi zitakuwa kati ya Sh. 1,770 kwa
mwezi mpaka Sh. 2,360.
Pia kwa watakaotumia ATM kutoa fedha, kila
watakapoingiza kadi kwenye mashine na kutoa
fedha, sasa watakatwa kati ya Sh. 944 mpaka
1,770 kutegemea na aina ya kati ambayo mteja
anaitumia.
KUPUNGUZA PAYE
Wakati akisoma hotuba ya bajeti bungeni Juni 8,
mwaka huu, Dk. Mpango alisema ili kuboresha
kipato cha wafanyakazi, serikali inapunguza kodi
ya mishahara (PAYE) kwa mishahara kutoka
asilimia 11 hadi asilimia tisa kwa wanaostahili
kulipa kodi hiyo kwa mujibu wa sheria.
Waziri huyo alisema watumishi wanaolipwa chini
ya Sh. 170,000, walikuwa hatozwi kodi, wakati
wale wenye mishahara ya zaidi ya Sh. 170,000
walikuwa wanatozwa kodi kulingana na makundi
yao ya mshahara kwa mujibu wa sheria.
Kodi ya PAYE kwa watumishi hupangwa na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwenye
makundi matano ya mishahara ya chini ya Sh.
170,000 (hawalipi kodi), Sh. 170,001 hadi 360,000
(walikuwa wakitozwa asilimia 11 ya kinachozidi
baada ya kutoa 170,000), wakati wenye mishahara
inayozidi Sh. 360,000 hadi 540,000 walikuwa
wanatozwa Sh. 20,900 jumlisha asilimia 20 ya
kinachozidi baada ya kutoa 360,000.
Wenye mishahara inayozidi Sh. 540,000 hadi
720,000 walikuwa wanatozwa 56,900 jumlisha
asilimia 25 ya kinachobaki baada ya kutoa Sh.
540,000, huku wale wanaolipwa zaidi ya Sh.
720,000 wakilipa Sh. 101,900 jumlisha na asilimia
30 ya kinachozidi baada ya kutoa 720,000.
PESA KUFICHWA MAJUMBANI
Profesa Lusato Kulwijira wa Chuo Kikuu cha Kilimo
(SUA), alisema jana kitendo cha benki kuongeza
gharama za miamala na huduma zake kitakuwa na
athari kubwa kwa wananchi wanaotegemea
huduma za kifedha za benki hizo.
Aidha, kutokana na kuongezeka huko kwa gharama
za huduma za kibenki, msomi huyo
alitahadharisha kuwa watu wengi watalazimika
kuhifadhi fedha kwenye nyumba zao na
kuhatarisha usalama wao.
"Ongezeko hili ni kuumiza mwananchi, hasa
mwenye kipato kidogo. Maisha ya mlaji wa
mwisho yatapanda sana.
Tulitegemea vitu vishuke bei, lakini kila kitu
kimepanda na watu hawana fedha," alisema
Profesa Kulwijira na kuongeza:
"Tunakoelekea watu wataficha fedha ndani ya
nyumba zao na wataanza kuvamiwa na kuibiwa."
Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Prosper
Ngowi, aliliambia gazeti la Nipashe kuwa ongezeko
hilo litaisaidia serikali kupata fedha na kuongeza
mapato yake lakini akatahadharisha kuwa huenda
watu wengi wataepuka kutumia huduma za
kibenki.
"Tutarudi kwenye 'cash economy' na kurejesha
wizi wa watu kuvamiwa majumbani. Huenda watu
wengi hasa wa kipato cha chini wakaachana na
utaratibu wa kutumia huduma za kibenki na
kuamua kutunza fedha zao wenyewe," alisema
Profesa Ngowi.
Alisema kiasi kilichoongezwa na serikali kwenye
mishahara ya watumishi kwa kupunguza Paye kwa
asilimia mbili ni kidogo mno kulinganishwa na
kodi ambazo wananchi wanaanza kutozwa leo.
"Ni kweli wamepunguza Paye hadi asilimia tisa,
lakini ukienda benki na kwenye kampuni za simu,
kodi ya miamala imeongezwa, ukienda kutalii,
unakatwa kodi.
Bajeti hii kila mtu itamwathiri kivyake," aliongeza
Profesa Ngowi.
Kwa hisani ya Nipashe, Imeandikwa na Fredy
Azzah na Sanula Athanas

Chapisha Maoni