0

WAZIRI wa mambo ya ndani ya nchi Mwigulu
Nchemba, amesema kuwa Serikali itahakikisha
inakabiliana kwa nguvu zote na tatizo la makazi
ya askari polisi nchini ili kulipa hadhi jeshi hilo
ambalo linakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Nchemba aliyasema hayo jana wakati alipokuwa
akizungumza na maafisa wa jeshi hilo pamoja na
askari wa kawaida wa mkoa wa Dodoma katika
kikao kazi kilichofanyika kwenye bwalo la jeshi
hilo mjini Dodoma.
Mwigulu alisema kuwa mojawapo ya suala
ambalo wizara yake italipa kipaumbele ni makazi
ya askari wa jeshi hilo ambayo mengi hivi sasa
yamechoka na kukosa hadhi ya kutumiwa na
askari wa jeshi hilo.
“Suala la makazi tutalipa kipaumbele kikubwa
sana na tutaanza hatua kwa hatua kulifanyia kazi
suala hili ili askari wetu waondokana na adha hii
wanayoipata kwa muda mrefu sasa,” alisema
Mwigulu.
Alisema kero nyingine watakayoifanyia kazi ni
kuhakikisha kuwa mazingira ya kufanyia kazi kwa
askari polisi yanaboreshwa kuanzia kazini kwao
na pia kwenye makazi yao.
“Kumekuwapo na tatizo la mafuta kwa jili ya
magari mnayoyatumia … hata tukio likitokea
mnashindwa kufika kwa kukosa mafuta.
"Pia kuna maslahi duni, umeme maofisini pamoja
na nyumbani mnapoishi imekuwa ni kero kubwa
kwenu hivyo sisi kama wizara tutahakikisha haya
yote tunayaondoa,” alisema Mwigulu.
Katika hatua nyingine, Mwigulu alitoa rai kwa
askari polisi nchini kuhakikisha kuwa
wanazingatia miiko ya kazi yao kwa kufanya kazi
kwa kuzingatia maadili kama ambavyo
walivyofundishwa katika mafunzo yao.
“Mimi uwepo wangu hapa sijaja kuwafundisha
kazi kwakuwa tayari kazi yenu mnaijua… ambayo
mmefundishwa mkiwa chuoni. Hivyo sisi kama
wizara jukumu letu ni kuweka mazingira wezeshi
ili mfanye kazi zenu katika mazingira mazuri,”
alisema.
Aidha alilitaka jeshi hilo kutumia nguvu katika
mahali panastahili tu kufanya hivyo ili hata
mwanachi akisikia utendaji wao ajivunie uwapo
wa jeshi hilo.
“Tumieni nguvu mahali mbapo Mtanzania wa
kawaida akisikia ajivunie uwapo wenu kama
ambavyo mmejitahidi katika suala la madawa ya
kulevya. Kama tutaweza kuubaini mnyororo huo
na kuukata, mwanchi wa kawaida atajivunia,”
alisema.
Aidha alisema kuwa jeshi hilo bado lina kazi
kubwa ya kufanya ili kukomesha mtandao wa
watu wanaojihusisha na madawa ya kulevya
nchini na pia akalitaka jeshi hilo kuhakikisha
linakuwa mtetezi wa wanyonge.
Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma, Lazaro
Mambosasa, awali akimkaribisha Waziri Mwigulu
alisema kuwa jeshi hilo limejipanga vilivyo katika
kuhakisha uhalifu unakomeshwa mkoani hapa.
“Mweshimiwa waziri mwenye utakuwa ni shahidi
ukiwa katika vikao vya bunge uliona namna
ambavyo amani na usalama ulikuwepo wa
kutosha. Hii yote ni kutokana na kujipanga vizuri
kwa jeshi la polisi mkoani hapa,” alisema
Mambosasa.



Posted Africa Newss

Chapisha Maoni

 
Top