BAO pekee la Ederzito ‘Eder’
Antonio Macedo Lopes
dakika ya 109, limetosha
kuipa Ureno ubingwa wa
kombe la Mataifa ya Ulaya,
maarufu kama Euro 2016
baada ya kuwafunga wenyeji
Ufaransa 1-0 Uwanja wa
Stade de France mjini Paris.
Katika mchezo huo
uliochezeshwa na refa Mark
Clattenburg wa England, Eder
aliyezaliwa mjini Bissau,
Guinea-Bissau, Desemba 22,
mwaka 1987 kabla ya
kuhamia Ureno alipotimiza
miaka 11 alifunga kwa shuti
la umbali wa mita 25 baada
ya kuingia kuchukua nafasi
ya Renato Sanches dakika ya
79.
Haukuwa ushindi mwepesi
kwa Ureno, kwani ilimpoteza
Nahodha wake Cristiano
Ronaldo aliyeumia dakika ya
25 na nafasi yake
kuchukuliwa na mkongwe
Ricardo Quaresma.
Ronaldo akarejea kwenye
benchi kuwasaidia makocha
wake kuwaongoza wachezaji
wenzake hadi kufanikiwa
kutwaa taji hilo.
Na kwa ushindi huo, Ureno
wanapata Euro Milioni 8,
wakati Ufaransa wanapata
Milioni 5, huku Ujerumani na
Wales wote wakipata Milioni
4 kila timu kwa kuishia Nusu
Fainali.
Timu zilizotolewa katika
Robo Fainali zitapata Euro
Milioni 2.5, wakati zilizoishia
16 Bora zitapata Milioni 1.5
na zilizopata ushindi katika
hatua ya makundi zinapata
Milioni wakati kwa kufuzu tu
kila timu inapata Euro
500,000
Hii ni mara ya kwanza kwa
Ureno kutwaa taji hilo, baada
ya awali kukomea Nusu
Fainali mara tatu katika
miaka ya 1984, 2000 na
2012, wakati Ufaransa ilikuwa
inajaribu kutwaa taji hilo kwa
mara ya tatu baada ya
mwaka 1984 na 2000.
Ureno ilianza Euro 2016 kwa
kusuasua baada ya kumaliza
mechi za Kundi F bila
ushindi ikitoa sare zote, 1-1
na Iceland, 0-0 na Austria na
3-3 na Hungary hivyo
kumaliza nafasi ya tatu
nyuma ya Hungary na
Iceland na kufuzu hatua ya
16 Bora kama mshindi wa
tatu bora wa makundi yote.
Katika hatua ya 16 Bora
ikashinda 1-0 baada ya
dakika 120, bao pekee la
mkongwe Ricardo Quaresma
dakika ya 117 na kwenye
Robo Fainali ikashinda kwa
penalti 5-3 baada ya sare ya
1-1 ndani ya dakika 120.
Ureno ikaustaajabisha
ulimwengu baada ya ushindi
wa 2-0 dhidi ya Wales ya
Gareth Bale katika Nusu
Fainali, mabao ya Nahodha
Cristiano Ronaldo dakika ya
50 na Luis Nani dakika ya 53
– kabla ya leo Eder kupeleka
taji la Euro 2016 Ureno.
Ufaransa inapoteza mechi ya
kwanza katika mashindano
haya, baada ya awali
kushinda mechi za Kundi A
dhidi ya Romania 2-1 na
Albania 2-0 kabla ya
kulazimishwa sare ya 0-0 na
Uswisi.
Katika hatua ya 16 Bora
iliwatoa Jamhuri ya Ireland
kwa kuwafunga 2-1, mabao
yake yote yakifungwa na
Antoine Griezmann huku la
wapinzani wao likifungwa na
Brady kwa penalti.
Katika Robo Fainali iliwatoa
Iceland kwa kuwachapa 5-2,
mabao yao yakifungwa na
Giroud mawili, Paul Pogba,
Payet na Griezmann huku ya
wapinzani yakifungwa na
Sigporsson na B. Bjarnason.
Na katika Nusu Fainali
waliwafunga Ujerumani 2-0,
mabao yote akifunga
mfungaji bora wa fainali za
mwaka huu, Griezmann
aliyemaliza na mabao sita
ambaye leo alifichwa na
mabeki wa Ureno.
Kikosi cha Ureno kilikuwa;
Rui Patricio, Cedric, Pepe,
Fonte, Guerreiro, William
Carvalho, Renato Sanches/
Eder dk79, Adrien Silva/Joao
Moutinho dk66, Joao Mario,
Nani na Ronaldo/Quaresma.
Ufaransa: Lloris, Sagna,
Koscielny, Umtiti, Evra,
Sissoko/A. Martial dk 110,
Pogba, Matuidi, Payet/K.
Coman dk58, Griezmann,
Giroud/A. Gignac dk78.
Posted Africa Newss
Chapisha Maoni