0
Serikali imeliagiza Jeshi la Polisi kukamatwa
viongozi wa kisiasa, wakiwamo wabunge
wanaofanya uchochezi na kusababisha uvunjifu wa
amani.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba bungeni jana,
wakati alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa
Ulanga (CCM), Godluck Mlinga, aliyetaka kujua
serikali inatoa kauli gani juu ya viongozi wa siasa
ambao wamekuwa wakitoa kauli za uchochezi na
kusababisha vurugu.
Mbunge huyo aliuliza swali hilo la nyongeza,
baada ya awali Mbunge wa Serengeti (Chadema),
Marwa Chacha, katika swali la msingi kutaka kujua
serikali inatoa tamko gani juu ya kuwapo kwa vifo
vya utata wa kisiasa.
Alidai kuwa inapotokea mpinzani kupoteza maisha
katika mazingira hayo, vifo hivyo huwa havipewi
kipaumbele katika upelelezi na hatua kuchukuliwa.
Swali hilo lilionekana kugusa hisia za wabunge
wengi ambao walisimama kuuliza maswali ya
nyongeza akiwamo Mlinga na Mbunge wa Mwibara
(CCM), Kangi Lugola, aliyetaka kujua Watanzania
na wabunge ambao wamekuwa na tabia ya
kuhusisha kila kifo na masuala ya kisiasa
wanachukuliwa hatua gani.
Alisema madai hayo yanaweza kuleta kutoelewana
katika jamii na kutaka yakomeshwe.
Naye Mbunge Viti Maalum (CCM), Angelina
Malembeka, alitaka kujua kama kuna ukweli
wowote kuhusu polisi kupiga raia katika kisiwa cha
Pemba, kwani anachofahamu jeshi hilo kazi yake ni
kulinda raia na mali zao.
Akijibu maswali ya nyongeza, Nchemba alisema
amewaagiza polisi kuhakikisha wanashughulika na
chanzo kwanza cha tatizo kwa kumkamata
kiongozi aliyewatuma wananchi wakafanye vurugu
au maandamano na uvunjifu wa amani, badala ya
kuwakamata wafuasi pekee.
Alisema Watanzania wote wanahaki sawa, hivyo
viongozi wanaowagawa wananchi kwa misingi ya
kisiasa na kuwatengenezea chuki wanapaswa
kupuuzwa.
Aliwaasa wananchi kutokubali kurubuniwa na
kutengenezewa chuki na wanasiasa ambayo
baadaye inawapelekea kupata matatizo.
“Uzoefu unaonyesha viongozi wamekuwa
wakiwachochochea wananchi na wanapopata
matatizo wanakuja hapa bungeni na kuongeana
glasi na wenzao, sasa nimeagiza waanze
kushughulikiwa wao,” alisema.
UDIKTETA
Kuhusu madai kuwa serikali inaongoza kidikteta,
Nchemba alikanusha madai hayo akisema
wanaolalamika ni wale waliozoea kuishi kwa
ujanjaujanja na kutofuata sheria za nchi.
“Natoa onyo kwa wale wote waliozoea maisha ya
kupiga dili kuachana na tabia hiyo na kufuata
sheria kanuni na taratibu za nchi ili waweze
kuisha kwa amani na utulivu,” alisisitiza waziri
huyo.
UCHOCHEZI
Awali akijibu swali la msingi, Naibu Waziri, Hamad
Yusuf Masauni, alieleza kuwa Jeshi la Polisi
limekuwa likitekeleza wajibu wake kwa mujibu wa
sheria na kanuni na halibagui mtu yeyote kwani
na linathamini Watanzania wote.
Alisema jeshi hilo limekuwa likichukua hatua
mbalimbali kwa viongozi wa vyama vya siasa
ambao wamekuwa wakisababisha vitendo vya
uvunjifu wa amani na uchochezi nchini ili
wananchi waweze kuishi kwa amani na utulivu.
“Iwe Mbunge au kiongozi wa chama cha kisiasa
atachukulia hatua kulingana na matendo
aliyoyafanya, Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya
Bunge inamlinda Mbunge kwa kile anachokisema
bungeni lakini si kwa matendo ya uhalifu
atakaoufanya nje,” alisema.
RAIA KUPIGWA PEMBA
Akijibu swali la Malembeka, Masauni alikanusha
polisi kupiga raia Pemba kama inavyodaiwa na
baadhi ya wanasiasa, akisema kuna mkakati wa
kupotosha jamii ili wawachukie polisi.
Alisema watu wanaokamatwa ni wale wanaofanya
vitendo vya uvunjifu wa amani wakiwamo viongozi
wa juu wa chama kimoja cha siasa ambacho
hakukitaja na kwamba wanahojiwa na watafikishwa
mahakamani.
DK. MWAKYEMBE APINGA
Baada ya Naibu Waziri huyo kujibu, alisimama
Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harson
Mwakyembe na kusema swali hilo la msingi la
Mbunge wa Serengeti halikupaswa kuingia bungeni
na kuulizwa, kwani limekiuka masharti ya kanuni
ya 40 ya kanuni za kudumu za bunge.
Alisema kanuni zinataka kupelekwa maswali
ambayo yana ushahidi ili serikali iweze kuyajibu
na si kuletwa kwa kubahatisha ndani ya bunge.
“Vifo vinavyozungumziwa kwenye swali hilo
havijathibitishwa kitaalam kama vinahusiana na
siasa, nawaonya viongozi hao wakiwamo wabunge
kutotumia siasa katika kuliendesha taifa kwani
haliwezi kujengwa kwa mtindo huo,” alisema.
DK. TULIA AMJIBU
Baada ya Waziri Mwakyembe kutoa kauli hiyo,
Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, alisema swali
lilipitiwa na kitengo cha sheria cha bunge na
kujiridhisha kwamba linastahili, hivyo wakati
mwingine serikali nayo ijiridhishe kabla ya kuleta
majibu bungeni.

Chapisha Maoni

 
Top