MBUNGE wa Vunjo ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Augustine Mrema (TLP),
amesema kuna haja Rais Jakaya Kikwete aongezewe muda wa kuongoza nchi.
Alisema kama Rais Kikwete ataongezewa muda, atapata muda wa kukamilisha mchakato wa Katiba
ambao ndiye aliyeuanzisha.
Mmoja wa wajumbe waliohudhuria kikao kati ya Rais Kikwete na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kilichofanyika mwanzoni mwa wiki Ikulu
ndogo ya Kilimani mjini Dodoma, aliiambia
MTANZANIA kwamba Mrema aliyasema hayo alipokuwa akichangia wakati wa kikao hicho. “Wakati mjadala unaendelea, Mrema alipendekeza
Rais Kikwete aongezewe muda wa mwaka mmoja
au miwili ili afanikiwe kukamilisha mchakato huu wa Katiba.
“Alipotoa pendekezo hilo, kuna mjumbe mmoja akamuuliza, ‘sasa Mrema unataka muda uongezwe ili na wewe upate muda wa kupambana
na Mbatia (James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi) anayekusumbua kule Vunjo au?’
“Huyo mjumbe alipouliza hivyo, Mrema akadakia na kusema, ‘hapo hapo’,” kilisema chanzo chetu kwa sharti la kutotajwa .
Chanzo hicho kilisema kuwa Mrema aliendelea kumsihi Rais Kikwete amzuie Mbatia asiende Vunjo kwa kuwa anapokuwa huko anatumia jina
lake, kwamba amemtuma kugombea ubunge wa jimbo hilo.
Mbatia alipozungumza na MTANZANIA kwa simu jana juu ya malalamiko hayo, alisema hawezi kuendelea kujibizana na Mrema kwa kuwa ni mkubwa wake.
“Mimi sikulelewa katika mazingira ya kujibizana na wakubwa zangu ila ninachosema ni kwamba,
wakati wa mkutano wangu wa hadhara
niliohutubia Vunjo wiki iliyopita, wenyeviti 11 wa serikali za vijiji walioshinda kupitia TLP, wenyeviti
32 wa vitongoni ambao ni wa TLP, msaidizi wa Mrema pamoja na wanachama wapya 1,564,
walihamia NCCR-Mageuzi,” alisema Mbatia.
Naye Mrema alipozungumza na MTANZANIA kwa simu, alikiri kutaka Rais Kikwete aongezewe muda
na kumwomba amzuie Mbatia kwenda Vunjo akidai kuwa anatumia jina la rais kumsema vibaya kwa wananchi.
Chanzo: Mtanzania
Chapisha Maoni