0
Mkakati wa kumdhibiti Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, katika mbio za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015, umeelekezwa kwa jamii ya wakulima na wafugaji hususani waliopo mikoa ya kanda ya Ziwa Victoria.

Hatua hiyo inadaiwa kufikiwa katika mkutano ulioratibiwa na Chama cha Wakulima wa Pamba (Tacoga) na kufanyika juzi katika ukumbi wa Benki
Kuu (BoT) jijini Mwanza. Pamoja na kulenga ajenda za changamoto
zinazowakabili wakulima, wafugaji na namna bora ya kuzishughulikia, mkutano huo unadaiwa kuelekezwa zaidi katika ‘kumshughulikia’ Pinda.

Akiwa jijini London, Uingereza hivi karibuni, Pinda alikaririwa akithibitisha kuwa miongoni mwa wanaotaka kuwania urais ili ‘kumrithi’ Rais Jakaya
Kikwete, ambaye ukomo wa utawala wake unafikia 2015.

Taarifa zilizolifikia NIPASHE Jumamosi zilieleza waratibu wa mtandao unaomuunga mkono ‘mgombea mwenye nguvu za fedha’ (jina tunalo),
waliutumia mkutano huo kama fursa ya kuibua chuki ya wakulima na wafugaji dhidi ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hususani Pinda.

“Pinda ameshughulikiwa kwa kukosolewa isivyostahili kupitia mkutano ili aonekane ni kiongozi aliyeshindwa kushughulikia kero za
wakulima,” alieleza mmoja wajumbe wa mkutano huo ambaye hata hivyo hakutaka jina lake kutajwa
gazetini.

Aliongeza, “lakini kwa kumshughulikia Pinda kwa niaba ya serikali, wanashindwa kutambua kwamba
wanaishughulikia serikali ya chama chao wenyewe.”
Chanzo hicho kilieleza mtandao unaomshughulikia Pinda ni wa ‘mgombea mwenye nguvu za fedha’,
ambao katika mkutano huo uliongozwa na baadhi ya wenyeviti wa CCM wa mikoa miwili, mmoja wa kanda ya ziwa na mwingine wa kanda ya kati.
Pia wamo baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM wanaotoka katika mikoa kadhaa nchini, walioalikwa kushiriki mkutano huo.

Lengo la kuugeuza mkutano wa wakulima na wadau wa kilimo hasa cha pamba na ufugaji lilielezwa ni kutaka kuibua hasira za wakulima na wafugaji kuichukia serikali, kwamba imeshindwa
kutimiza wajibu wake katika kuwatatulia kero zao.

Kwa hali hiyo, mtazamo huo unaelekezwa moja kwa moja kuzishawishi jamii hizo kuwataka
wabunge wao ‘kumbana’ Pinda katika mkutano wa Bunge unaotarajiwa kuanza mwezi ujao mjini Dodoma, ikibidi kumtaka ajiuzulu.

“Huwezi ukamchafua Waziri Mkuu kwa kashfa ambazo mhusika mkuu ni serikali ya chama chako, hata kama Pinda atastahili kulaumiwa, matokeo yake itakuwa ni kupunguza kura za CCM
kwenye ukanda huo na jamii zilizoshiriki,” kilieleza chanzo kingine kutoka ndani ya mkutano huo.

Kumekuwa na hujuma nyingi zinazoripotiwa kuelekezwa kwa Pinda, ambapo katika mkutano wa Nec uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma,
taarifa zilichapishwa na kutangazwa kuhusu kushamiri kwa rushwa iliyowalenga watu wanaomuunga mkono.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa CCM
walioalikwa katika mkutano huo, Mgana Msindai (Mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM) na Mweyekiti wa chama hicho mkoa wa Shinyanga, Hamis
Mgeja, hawakupatikana kwenye simu zao kuzungumzia hayo.

Lakini, akizungumzia na NIPASHE Jumamosi, Mwenyekiti wa Tacoga, Elias Zizi, alipingana na taarifa hizo na kudai ulikuwa Mkutano Mkuu wa
kikatiba usiohusika na masuala ya siasa.
“Haukuwa mkutano wa kumjadili yeyote, bali ni kwa ajili ya kufahamu changamoto na mafanikio anayokabiliana nayo mkulima wa pamba…
tulikaribisha wageni mbalimbali ambao ni wadau wa zao hilo,” alisema Zizi.

Kwa upande mwingine, vyanzo vingine viliwakariri baadhi ya viongozi wa CCM waliohudhuria, wakisema wapo tayari kumshughulikia Pinda kwa
vile kufanya hivyo hakukiathiri chama hicho.
“Nilimsikia (anamtaja jina) akitoa mfano kuwa kumshughulikia Abdallah si kuushughulikia msikiti ama kumshughulikia Joseph si kulishughulikia Kanisa, hivyo Pinda anastahili kushughulikiwa kwa
vile hakuiathiri CCM,” kilieleza chanzo kingine. Hivi karibuni, kumekuwapo madai ya kuhujumiwa
kwa Pinda, ikiwamo matumizi ya rushwa kwa wajumbe hasa wa Nec wanaomuunga mkono.

Inaelezwa kuwa wajumbe kutoka makundi yanayowaunga wanachama wengine wa CCM wenye nia ya kuwania urais, wamekuwa wakijiunga na kumuunga mkono Pinda, hali
iliyobadilisha upepo wa kisiasa ndani ya chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015.



CHANZO: NIPASHE

Chapisha Maoni

 
Top