Matumaini ya eneo la Afrika Mashariki kuwa na timu angalau moja katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika nchini Equatorial Guinea
mwaka 2015, yameyeyuka baada ya mwakilishi pekee wa eneo hilo timu ya Uganda kucharazwa na Guinea mabao 2-0 katika mchezo wa kundi E uliofanyika mjini Casablanca, Morocco, Jumatano. Uganda iliyokuwa na pointi 7 kama Guinea ilitakiwa kushinda mchezo huo.
Ghana inaongoza kundi hilo
ikiwa na pointi 11. Katika kundi hilo Ghana imeicharaza Togo 3-1. Timu za Uganda na Togo zimeaga michuano hiyo.
Mabingwa wa zamani wa michuano hiyo kwa mwaka 1968 na 1974, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (Zaire), imefanikiwa kutinga katika michuano ya
mataifa ya Afrika mwakani kwa kuwa na wingi wa pointi kati ya timu zote zilizoshika nafasi ya tatu katika makundi yote nane. DR Congo imeibuka na
pointi 9.
Mabingwa watetezi Nigeria imetupwa nje ya michuano hiyo baada ya kutoka sare na Afrika Kusini kwa kufungana mabao 2-2. Nigeria imebaki na pointi
8.
Timu zilizofuzu kutoka kila kundi ni kama ifuatavyo:
Kundi A: Afrika Kusini yenye pointi 12 na Congo pointi 10. Nigeria na Sudan zimetupwa nje.
Kundi B: Algeria na Mali zimesonga mbele kwa alama 15 na 9 kama zinavyofuatana, huku Angola na
Lesotho zikifungasha virago.
Kundi C: Gabon na Burkina Faso zimetinga hatua ya fainali kwa kujikusanyia alama 12 na 11 kama
zinavyofuatana.
Kundi D: Cameroon, Ivory Coast na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo zina pointi 14, 10 na 9 kama zilivyoongozana. Sierra Leone imetupwa nje.
Kundi E: Ghana na Guinea kwa alama 11 na 10. Uganda na Togo zimeyaaga mashindano hayo.
Kundi F: Cape Verde na Zambia zenye pointi 12 na 11 zikiziacha timu za Msumbiji na Niger.
Kundi G: Senegal na Tunisia zina pointi 13 na 14. Misri na Botswana zimeshindwa kufuzu, pale zilipoambulia pointi 6 na 1 kama zinavyofuatana.
Fainali hizi za Kombe la Mataifa ya Afrika zinafanyika nchini Equatorial Guinea ambayo nayo imepewa
nafasi kutokana na kuwa nchi mwenyeji wa michuano, baada ya Morocco iliyokuwa imepewa nafasi ya kuandaa kutaka michuano hiyo kuahirishwa
kwa hofu ya ugonjwa wa Ebola ambao umeziathiri nchi za Afrika Magharibi, hususan Liberia, Sierra
Leone na Guinea.
Vigogo wa soka barani Afrika, Nigeria na Misri hazitaonekana katika fainali hizo.
Chapisha Maoni