Wanafunzi 297,488 wa kidato cha nne wanaanza mtihani wa kuhitimu elimu ya sekondari utakaokamilika baada ya siku 20, huku watahiniwa wakionywa kujiepusha na vitendo vya udanganyifu.
Idadi ya watahiniwa wa mwaka huu ni pungufu ikilinganishwa na ya mwaka jana wakati walipokuwa wanafunzi 367,399.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama alisema juzi kwamba kati ya idadi hiyo, watahiniwa wa shule ni 245,030 na watahiniwa wa kujitegemea ni 52,458.
Kati ya watahiniwa wa shule, wavulana ni 132,244 sawa na asilimia 53,97 na wasichana ni 112,786 sawa na asilimia 46.03.
Mhagama alisema kati ya watahiniwa wa kujitegemea 52,458, wanaume ni 25,458 na wanawake ni 26,684.
Alisema kati ya watahiniwa hao, 51 ni wasioona wakiwamo wavulana 37 na wasichana 14 na kwamba wenye uoni hafifu ambao huhitaji maandishi makubwa ni 356.
Alisema watahiniwa waliojiandikisha kufanya mitihani ya maarifa ni 14, 723 na kati ya wanaume 5,940 na wanawake 8,783.
Mhagama alizitaka mamlaka mbalimbali
kuhakikisha kwamba zinazuia udanganyifu katika mtihani huo.
“Maofisa elimu na mikoa na kwenye halmashauri hakikisheni taratibu zote za mitihani zinafuatwa, zuieni mianya yote inayoweza kusababisha udanganyifu,” alisema.
Mhagama alisema wanafunzi watakaobainika kufanya udanganyifu, watachukuliwa hatua ikiwemo kufutiwa mtihani.
Chapisha Maoni