Ripoti ya sakata la uchotaji wa Dola za Marekani 200 milioni katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyotua bungeni wiki iliyopita, imeibua mambo mazito baada
ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kugundua kuwa fedha zilizochotwa kwenye akaunti hiyo zilikuwa mali ya Tanesco.
Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali zinaeleza kuwa fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo ni Sh306 bilioni wakati madai ya Tanesco kwa IPTL ni Sh321
bilioni, hivyo fedha zote za Escrow zilipaswa kwenda Tanesco na bado ingekuwa inadai.
Ukaguzi wa akaunti hiyo uliamuliwa na Serikali baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR- Mageuzi), David Kafulila kudai kuna ufisadi katika uchotaji wa fedha hizo katika Benki Kuu ya Tanzania
(BoT).
Akaunti hiyo ilifunguliwa baada ya kutokea mgogoro wa kibiashara baina ya Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco) na Kampuni ya kufua umeme ya IPTL. Katika mgogoro huo, Tanesco ilikuwa inabishia kiwango cha fedha ilichokuwa inalipa kwa gharama
za uwekezaji kwa IPTL, ndipo ikaamuliwa na mahakama ifunguliwe akaunti hiyo ili fedha ilizokuwa
inalipa ziendelee kuwekwa huko hadi mgogoro utakapokwisha.
Kesi hiyo iliamuliwa katika mazingira yanayoelezwa kuwa na utata na fedha hizo kuchukuliwa haraka na
IPTL. (P.T) Baada ya ripoti ya uchunguzi huo kukabidhiwa bungeni wiki iliyopita chanzo chetu kimeeleza kuwa kwa mujibu wa ripoti hiyo fedha ni za umma na zilipaswa kwenda Tanesco na shirika hilo kuendelea kuidai IPTL Sh15 bilioni.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Kampuni ya PAP haikununua kihalali asilimia 70 ya hisa za Kampuni ya Mechmar katika IPTL kwani zilizuiliwa na mahakama, hivyo hawana hati halisi ya hisa na
kwamba ilifanya udanganyifu katika malipo ya kodi kwa kutoa nyaraka za uongo kuwa walinunua hisa
kwa Sh6 milioni badala ya Dola za Marekani 20 milioni, hivyo kuikosesha Serikali Sh8.7 bilioni.
Pia imeeleza kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alivunja sheria kwa kuelekeza kuwa kodi ya ongezeko la thamani kwenye gharama za uwekezaji
isilipwe na hivyo kusababisha Serikali kupoteza mapato ya Sh21 bilioni.
"Wizara ya Nishati na Madini haikufanya uchunguzi wa awali (due diligence) kuhusu uhalali wa umiliki wa Kampuni ya IPTL na ilisaini kutoa fedha bila ya
kuhakikisha fedha za Tanesco zinarudi na hivyo kusababisha kulipotezea Shirika zaidi ya Sh321
bilioni," chanzo chetu kilieleza.
Hata hivyo, Naibu Spika, Job Ndugai alipoulizwa juzi baada ya kutoka kwenye Kamati ya Uongozi, bila kufafanua alisema ripoti itawasilishwa bungeni
Novemba 26, mwaka huu kama ilivyopangwa na kuwa angetoa taarifa ya kilichojiri kwenye Kamati ya
Uongozi bungeni leo.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Uongozi wameeleza kuwa, wamekubaliana ripoti hiyo iwasilishwe kama ilivyopangwa na kwamba muda
huu ofisi ya Katibu wa Bunge na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) waipitie kwa ajili ya uwasilishwaji.
Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Zitto Kabwe ambaye ameshakabidhiwa ripoti hiyo alipoulizwa alisema bado anaipitia ripoti hiyo kwa kuwa ina kurasa zaidi
ya 300.
"Namshukuru sana CAG kwa kumaliza kazi hii na kujibu hadidu za rejea zote. Ni taarifa kubwa yenye zaidi ya kurasa 300," alisema Zitto.
Hadidu za rejea Katika uchunguzi huo, CAG alipewa hadidu za rejea
za kuchunguza uendeshaji wa mkataba wa kuzalisha umeme kati ya Kampuni ya IPTL na Tanesco, pia kuchunguza kama wakati escrow inafunguliwa
Kampuni ya Mechmar ilikuwa inamiliki IPTL, kama ilikuwa imefilisiwa au iwapo ilikuwa imehamisha umiliki wake kwa Kampuni ya PAP.
Vilevile kuchunguza na kuthibitisha ushahidi wa Kampuni ya PAP kununua Kampuni ya Mechmar na kumiliki IPTL na chanzo cha mgogoro kuhusu tozo
kati ya Tanesco na IPTL na kuthibitisha ushahidi wowote kuwa mgogoro uliamuliwa kwa faida ya
IPTL.
Lingine ilikuwa ni kuchunguza iwapo ilikuwa sahihi kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kusamehe kodi ya VAT ya jumla ya Sh26 bilioni kutokana na tozo ya capacity charges na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wachukue hatua gani kuhakikisha kodi hiyo
inakusanywa.
Pia kuchunguza kiwango cha fedha kilichopaswa kuwamo katika akaunti ya escrow, kiwango gani kilikuwapo wakati IPTL wanalipwa na kiwango gani
kitapaswa kulipwa zaidi kutoka Tanesco.
Vilevile kuchunguza madai ya Benki ya Standard Chartered kwa Tanesco na madai mengine yoyote yanayohusiana na mkataba wa kuzalisha Umeme wa
IPTL na iwapo Serikali imejihadhari na uwezekano wa madai yanayoweza kufunguliwa, nafasi na heshima
ya nchi katika kuheshimu mikataba ya kimataifa na ya uwekezaji.
Pia alitakiwa kuchunguza iwapo Wizara ya Nishati na Madini ambayo ni mhusika mkuu wa akaunti ya escrow ilifanya 'due diligence' ya kutosha kabla ya kuingia makubaliano ya kutoa fedha zilizopo kwenye akaunti.
Kutoa mapendekezo ya njia bora za kisheria kulinda Taifa kutoingia hasara zaidi katika mkataba wa IPTL
chini ya wamiliki wapya na kutoa ushauri kwa kamati ya PAC juu ya mapendekezo ya hatua ambazo Bunge
linapaswa kuchukua kuhusu matokeo ya ukaguzi huu maalumu.
Chanzo:Mwananchi
Chapisha Maoni