Ilikuwa ni hekaheka, patashika nguo kuchanika, wakati risasi na mabomu ya machozi ziliporindima kutoka kwa Jeshi la Polisi kuwatawanya wananchi waliokuwa wakichota mafuta yaliyomwagika kutoka kwenye lori la
mafuta aina ya scania lililopata ajali.
Sinema ilianza saa tatu usiku wa kuamkia jana baada ya lori hilo lililobeba shehena ya mafuta ya petroli, kushindwa kupanda mlima, kuserereka
kisha kupinduka, eneo la Tabata Kisiwani kwa Mama Pindapinda.
Baada ya ajali hiyo, mafuta yalianza kumwagika na kuwavutia wakazi wa jirani na eneo hilo waliobeba vyombo mbalimbali yakiwamo mabeseni na ndoo za maji ili kuchota nishati
hiyo.
Mjumbe wa Mtaa Bonde la Mchicha, Tabata Kisiwani, Mama Pindapinda alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Alisema kwamba alipiga simu polisi kuwataarifu na walifika, lakini baada ya gari hilo kuondolewa eneo la tukio, polisi nao waliondoka usiku wa saa 8.
Alieleza kuwa na baada ya hapo, wakazi hao waliendelea kuchota mafuta na kusababisha magari kushindwa kupita eneo hilo hali iliyosababisha mtaa huo kufungwa kabisa.
Waendesha bodaboda kutoka kila kona ya mitaa ya Tabata, walikusanyika na kujaa eneo hilo ili kununua mafuta kwa bei nafuu na wengine kuamua kuvaa nguo za kazi na kujichotea petroli
hiyo.
“Nimeamka saa kumi usiku kuchota mafuta na nimeyauza ya Sh20,000,” alisema mwanamke mmoja aliyekuwa eneo hilo akiwa amelowa mafuta
mwili mzima.
Hadi kufikia saa 3 asubuhi, waendesha bodaboda waliendelea kumiminika eneo hilo, wengi wakiwa na chupa kubwa za maji ya uhai, madumu ya lita
20 na yenye ujazo wa lita tano wakisomba mafuta hayo.
Sehemu yalipomwagika mafuta hayo, yalionekana mashimo mfano wa visma, vilivyochimbwa na wakazi hao kwa ajili ya kupata mafuta.
Mtaa huo na maeneo jirani, yalitawala harufu ya petroli, huku baadhi ya wakazi wake wakiamua kuzima umeme na kutowasha moto kuhofia kutokea kwa mlipuko.
Hata hivyo, tafrija hiyo ya mafuta haikudumu kwa muda mrefu, kwani ilipofika saa tano asubuhi, kundi la Jeshi la Polisi na Askari wa Kikosi cha
Kutuliza Ghasia(FFU), walifika eneo hilo na kuanza kuwatawanya wakazi hao kwa risasi, ambapo walianza kukimbia huku na kule.
Risasi hizo ziliwatawanya pia waendesha bodaboda walioanza kukimbia na vyombo vilivyojaa mafuta, huku baadhi wakizitelekeza
pikipiki zao.
Kutokana na hali hiyo, polisi hao waliamua kuzichukua pikipiki zilizotelekezwa, huku wakizivunja baadhi na kusababisha heka heka zaidi na hofu kutanda eneo hilo.
Vurumai hizo zilileta madhara hata kwa majirani wa lilipotokea tukio, kutokana na risasi kuathiri nyumba zao kwa kuvunjika vioo na kusababisha
nyufa kwenye kuta za makazi yao.
“Risasi imeingia ndani, tena hapa ambapo mtoto huwa analala. Imevunja kioo na kuharibu kabisa dirisha, “ alisema Adam Kihiki mkazi wa eneo hilo.
Mpaka saa 7 mchana jana, bado polisi
walionekana kutanda eneo hilo ili kuwazuia wananchi wa eneo hilo, ambao walionekana bado wana uchu wa kuchota mafuta hayo yaliyomwagika baada ya gari lililobeba kupinduka.
Chapisha Maoni