Habari kutoka Rukungiri, Uganda zinasema kuwa mtoto mdogo wa miaka miwili aliyekuwa mgonjwa, amenusurika kifo baada ya kupata kipigo kutoka kwa dada wa kazi, Jolly Tumuhiirwe
(22), aliyekuwa akimlisha.
Jolly alimpiga mtoto huyo Jumamosi iliyopita wakati akimlisha mtoto huyo aliyekuwa mgonjwa, baada ya kushindwa kula haraka kama
alivyotarajiwa na kutapika.
Bila kujua kuwa nyumba hiyo ilikuwa na kamera ya usalama liyokuwa ikichukua matukio yote, Jolly aliyeanza kazi katika nyumba hiyo miezi mitatu iliyopita, aliamua kunywa uji wa mtoto huyo baada ya kuona mtoto mwenyewe hawezi kunywa kwa haraka.
Picha ya sekeseke hiyo ilitembea sana katika mitandao ya kijamii juzi, watu wakibadilishana kwa kasi ya ajabu.
Wakati akinywa uji huo, picha hiyo iliyosambaa katika mitandao ya jamii juzi , ilionesha Jolly akimpiga vibao mtoto huyo kabla ya kumtupa chini akiangukia uso, kutoka katika kochi la sofa.
Wakati mtoto huyo akiwa chini amelala kwa tumbo, Jolly akitumia mkono wa tochi, alianza kumpiga mtoto huyo katika makalio yake akiwa hana nguo yoyote.
Kama vile hakuridhika na kipigo hicho, dada huyo wa kazi aliamua kumpiga mtoto huyo mateke na baadae aliamua kumkanyanga kiunoni kwa mguu
wake.
Picha hiyo imeeonesha namna dada huyo alivyompiga mtoto huyo kwa teke kwa mara nyingine, kabla ya kumnyanyua kwa mkono mmoja na kumuingiza katika chumba kingine.
Taarifa kutoka katika familia ya mtoto huyo, zilizoripotiwa na mtandao wa The investigator today, imeeleza kuwa baba wa mtoto huyo, Erick Kamanzi, aliporejea nyumbani alibaini kuwepo kwa michubuko katika maeneo ya nyuma ya mwanaye.
Kabla ya kuuliza kilichotokea, Kamanzi alikimbilia chumbani kwake kupitia video na kuona kilichofanyika, ambapo alimvamia Jolly na kuanza kumpiga na baada ya kumaliza hasira zake,
alirejea kwa mwanaye ili kumsaidia.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, dada huyo wa kazi aliamua kukimbilia Kituo cha Polisi Kiwatule, ambako aliripoti tukio la kuvamiwa na kupigwa na mwajiri wake na askari Polisi walifika nyumbani
na kamkamata Kamanzi.
Akiwa kituo cha Polisi, taarifa za Polisi zinasema Kamanzi alikiri kosa na kuwekwa ndani na baada ya muda, aliwaomba askari hao kuangalia picha
za video zilizosababisha ampige msichana huyo wa kazi, hatua iliyosababisha askari Polisi
kumuachia mara moja.
Akizungumza na mtandao wa The investigator today, Msemaji wa Jeshi la Polisi la Uganda, Kamishna wa Polisi, Fred Enanga, alikiri kuwa Jolly ameshafunguliwa mashitaka katika
Mahakama ya Nakawa juzi kwa kosa la kukiuka Sheria ya Kuzuia Mateso.
Hata hivyo, Kamishna Enanga aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linajiandaa kubadilisha mashitaka ili yawe ya jaribio la kuua.
Kamishna Enanga alisema Jolly atafikishwa tena mahakamani Desemba 8, 2014. Juhudi za mtandao huo kupata maelezo ya mama wa mtoto huyo, Angella ambaye ni raia wa Rwanda,
hazikufanikiwa, kwa kuwa chanzo cha habari kilikataa kuzungumzia hilo.
Chapisha Maoni