SPIKA wa Bunge, Anne Makinda amewaambia wabunge kuwa vitendo vyao vya kukubali kurubuniwa kwa rushwa na baadhi ya wafanyabiashara, watajikuta wanakwenda ndani na
Bunge halitawatetea.
Akizungumza kabla ya kuahirishwa kwa Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge mjini Dodoma juzi, Makinda aliwataka wabunge kuachana na watu wanaofanya ushawishi kwa kutumia fedha.
Alisema vitendo hivyo, vinawaaibisha na
vitawaondolea uadilifu wao katika kuisimamia Serikali. “Kuna hili la lobbying (ushawishi) linalofanywa na
wafanyabiashara. Acheni kupokea rushwa, mtaaibika. Kama ninyi sio wasafi, mtawezaje kuwasimamia wengine,” alisema Makinda.
“Hakika mtajikuta mko ndani, na sisi hatutakuja kuwasaidia. Kama chombo hicho cha kuwasimamia wananchi kitaoza, nani atawasimamia wananchi? “Wananchi wanatutegemea sisi kwa hiyo acheni vitendo hivyo, vitawaaibisha na mtatiwa ndani na mimi sitakuja kuwatoa. Kataeni vitendo hivyo,” alisema
Spika Makinda.
Kauli yake imekuja baada ya kuwapo kwa madai ya matumizi makubwa ya rushwa katika sakata la akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya
Tanzania (BoT), ambayo ilikuwa mali ya Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania
Limited (IPTL).
Wakati wa majadiliano ya sakata hilo linalohusisha uchotaji wa Sh bilioni 306 zilizokuwa katika akaunti hiyo, baadhi ya wabunge waliwatuhumu wenzao kwa kuhongwa kufanikisha njama za ama
kuwatetea watuhumiwa au kuwakandamiza watu wasiohusika.
Miongoni mwa waliohusishwa na sakata hilo ni viongozi wa umma, watendaji wa serikali, wafanyabiashara, majaji, ambao inaaminika kwa namna moja au nyingine walihusika kufanikisha uchotaji huo wa fedha na wengine kunufaika na
fedha hizo.
Chapisha Maoni