Mnamo tarehe 4 Desemba 2014, Gazeti la Raia Tanzania, Toleo Na.0259 liliandika habari iliyokuwa na kichwa cha habari “Waziri Muhongo ‘atimkia’ Norway”.
Gazeti hilo lilieleza kwamba Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ambaye anapaswa kuwajibishwa kwa mujibu wa ushauri
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, yuko kikazi nchini Norway ambako ameongozana na viongozi
waandamizi wa Wizara yake.
Wizara inatoa taarifa kwa Watanzania kwamba habari hiyo haina ukweli wowote kwani Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
yupo hapa nchini na tarehe ambayo gazeti husika lilichapisha habari hiyo, Mhe. Muhongo alikuwa wilayani Musoma, mkoani Mara kuhudhuria hafla
ya kuwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri kwenye masomo katika shule ya Msingi ya Mwisenge A na B.
Waziri Muhongo alihudhuria hafla hiyo baada ya kualikwa na Ubalozi wa China hapa nchini, ambao umetoa ufadhili wa masomo na zawadi kwa wanafunzi walemavu wapatao 108 waliofanya
vizuri katika masomo yao. Aidha, Ubalozi wa China umetoa ufadhili wa kuwapeleka baadhi ya wanafunzi kutoka katika shule hizo kwenda nchini
China kwa lengo la kujifunza utamaduni wa nchi hiyo.
Ufadhili huo wa masomo umetolewa na Ubalozi wa China kwa ajili ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwl. Julius. K. Nyerere ambaye alisoma katika
shule hiyo.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Balozi Mdogo wa Ubalozi wa China Bw. Li Xuhang, Meya wa Mji wa Musoma Mhe. Alex Kisulura, Mhe. Madaraka
Nyerere, Bw. Joseph Kahama pamoja na walimu na wanafunzi wa shule hizo.
Tunapenda kuwakumbusha waandishi wa habari kuzingatia maadili ya taaluma na uzalendo ikiwa ni pamoja na kuandika habari zilizofanyiwa uhakiki
na zenye ukweli, zisipotoshe Umma ili kuondoa usumbufu kwa wananchi.
Imetolewa na,
WIZARA YA NISHATI NA MADINI
5 Desemba 2014
Chapisha Maoni