Baada ya Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumaliza mjadala wa sakata la Escrow, maelfu ya waumini wa madhehebu mbalimbali
mkoani Arusha wamefanya ibada maalumu ya kuliombea taifa amani na pia kuwaombea watendaji wa serikali na wananchi kwa ujumla kumtanguliza Mungu kwa kila wanalolifanya.
Wakizungumza katika ibada hiyo iliyofanyika katika uwanja wa magereza ulioko Kisongo nje kidogo ya jiji la Arusha viongozi wa ibada hiyo
akiwemo muhubiri Joven Abel Msuya kutoka taasisi ya huduma ya safina amesema pamoja na hatua na maamuzi yaliyofikiwa katika mjadala uliokuwa unaendelea pande zote zinahitaji
kuombewa ili hofu ya mungu iendelee kutawala na haki iweze kutendeka amani iendelee kutawala .
Muhubiri Abel amesema yote yaliyotokea na yanayoendelea kutokea ni matokeo ya kutenda mambo bila kumtanguliza mungu na kwamba njia
pekee ya kuepuka vitendo hivyo kuendelea kujitokeza ni kudumisha maombi na amewaomba watanzania kila mmoja kwa imani yake kuona
umuhimu wa kuliombea taifa amani.
Kwa upande wao baadhi ya waumini wamesema maovu yanayoendelea kutokea yanaonesha wazi kuwa lipo tatizo kubwa ambalo halijapata
ufumbuzi na yanadhihirisha kuwa bado kuna changamoto kubwa kwa viongozi wa serikali, viongozi wa kiroho na wananchi kwa ujumla ya kukabiliana na maovu .
Chapisha Maoni