0
Huku wanadiplomasi wa matiafa ya
magharibi wakiwa na wasiwasi kuhusu
mustakabali wa Burkina Faso, raia wa
nchi hiyo wanaliunga mkono jeshi
kuongoza mchakato wa mageuzi katika
taifa hilo.Huku baadhi ya wanadiplomasia wakiwa
wameeleza wasiwasi wao kuhusu jukumu la jeshi katika siasa tangu maandamano yaliyomuangusha madarakani rais wa muda mrefu Blaise Compare mwezi Oktoba mwaka huu, ni Waburikabe
wachache tu wenye wasiwasi mkubwa
kuhusu jeshi kuendelea kuyalinda
mapinduzi yao na kuruhusu mageuzi
muhimu waliyoyadai.

Wakati kanali Isaac Zidda alipoyavua
magwada yake ya kijeshi na kuvaa suti
kuwa mwenyekiti wa mkutano wa
kwanza wa baraza la mawaziri kama
waziri mkuu wa Burkina Faso, huenda
alitaka kutuma ujumbe kwa nchi za
Magharibi na washirika wa barani Afrika.

Ingawa watu kadhaa waliuwawa kwa
kupigwa risasi wakati wa mapinduzi ya
Burkina Faso, kanali Zida alizikonga nyoyo za waandamanaji wakati wanajeshi wa kikosi cha ulinzi wa rais alichokuwa akikiongoza kilipokataa kuufyetulia risasi umati wa watu waliokuwa wakiingia katika jengo la bunge.

Alishangiliwa kama shujaa
alipowahutubia waandamanaji katika
uwanja wa uhuru, kiasi cha
kulinganishwa na shujaa wa mrengo wa
shoto Thomas Sankara aliyeitawala
Burkina Faso kati ya mwaka 1983 na 1987.

"Ukiona tunaendelea kufanya kazi na
wanajeshi hawa leo, ni kwa sababu
walifanya kazi yao ya kulinda badala ya
kuwapiga risasi raia," alisema Michel
Kafando, rais mpya wa mpito wa Burkina
Faso, ambaye baraza lake lina mawaziri
sita ambao ni maafisa wa jeshi.

"Watabaki na sisi kwa kuwa
wamedhihirisha utiifu wao kwa raia.
Vinginevyo tungetumbukia katika vita vya
wenyewe kwa wenyewe," akaongezeka
kusema rais huyo katika mahojiano
aliyofanyiwa na televisheni ya Ufaransa,
France 24.

Zida analionyesha jeshi la Burkina Faso
kama mlinzi wa mapinduzi. Anaahidi
kufanya mageuzi pamoja na
kuvichunguza visa vya rushwa na vifo
vilivyotokea katika mazingira
yasiyoeleweka wakati wa enzi ya
Compaore.

Zida ameshawahi kuliambia taifa kwamba wizara ya sheria itakuwa na kibarua kikubwa na kigumu na itakuwa na jukumu muhimu wakati wa kipindi cha mpito.

Kuingia jeshi madarakani kulitokea kwa
bahati mbaya. Viongozi wa upinzani wa
Burkina walisita kutoa miito kutaka
Campaore aondolewe madarakani hata
katika wakati ambapo maandamano
yalikuwa yakipamba moto kupinga
jitihada zake za kuibadili katiba ili aweze
kugombea tena wadhifa wa urais katika
uchaguzi mwakani.

Mambo yalibadilika kwa haraka kuliko
mahasimu wa Compaore walivyodhania.
Baada ya Compaore kusitisha kura kuhusu mageuzi ya katiba, makundi ya watu waliandamana kuelekea ikulu yake na kumlazimisha ang'atuke. 

Katika makao makuu ya chama chake katika mji mkuu Ouagadougou, bia na chakula kilichokuwa kimeandaliwa kwa ajili ya sherehe baada ya mageuzi ya katiba kupitishwa, kililiwa na waandamanaji waliojawa na
ghadhabu.

"Viongozi wa kisiasa hawakuwa tayari.
Vijana waliendeleza shinikizo na jeshi
lilifanya vile watu walivyotaka," amesema Luc Marius Ibriga, profesa wa sheria na kiongozi wa jumuiya ya kiraia.

"Tungependelea kuwa na serikali ya
kiraia, lakini hii ndio hali halisi ya kisiasa
Burkina Faso," akaongeza kusema profesa huyo.

Pascal Marie Iliboudo, mwanachama wa
chama wa MPP, amesema anaunga mkono miito ya Zida kutafuta haki kwa uhalifu uliotendwa wakati wa utawala wa Compaore, lakini akasema kanali huyo hatakiwi kuruhusiwa kuzoweya utamu wa madaraka.

Profesa Ibriga amesema viongozi wa
Burkina Faso hawakuelewa ushauri wa
mabalozi wa nchi za kigeni waliosema
Compaore alipanga kurefusha utawala
wake wa miaka 27, lakini wakaingilia kati
kuwashauri jinsi ya kusimamia kipindi
cha mpito na kurejesha madaraka wa
utawala wa kiraia.

Rinaldo Depagne, Mkuu wa shirika la
Kimatiafa linaloshughulikia mizozo, ICG,
kanda ya Afrika Magharibi, amesema
yumkini kukatokea mivutano kati ya
vyama vinavyotaka uchaguzi ufanyike
haraka iwezekanavyo na makundi
mengine yanayotaka mageuzi yapewe
kipaumbele.

Serikali mpya ya Burkina Faso inakabiliwa na uhaba wa fedha huku athari za mapinduzi zikianza kuathiri uwekezaji na hazina za serikali kuanzia kodi hadi mauzo ya dhamana. Depagne amesema viongozi wanatakiwa waamue
wanachotaka kukifanikisha.


Mwandishi: Nyamiti Kayora/RTRE
Mhariri: Josephat Charo

Chapisha Maoni

 
Top