TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Profesa Mussa Juma Assad kuwa Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Taarifa iliyotolewa leo, Jumatatu, Desemba Mosi, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, inasema kuwa uteuzi wa Bwana Assad ulianza Novemba 5, mwaka huu, 2014.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Bwana Assad ataapishwa kesho, Jumanne, Desemba 2, saa nne asubuhi, Ikulu, Dar es Salaam.
Kabla ya uteuzi wake, Bwana Assad alikuwa Profesa Mshiriki, Idara ya Uhasibu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na anachukua nafasi ya Bwana
Ludovick Utouh ambaye amestaafu kwa mujibu wa Sheria za Utumishi wa Umma.
Profesa Assad ni msomi, mwenye weledi, ujuzi na uzoefu mkubwa wa uhasibu na udhibiti wa fedha
ambaye ana Shahada ya Uzamivu wa Uhasibu (PHD in Accounting) kutoka Chuo Kikuu cha Southampton, Uingereza mwaka 2001 na Shahada ya Uzamivu katika Udhibiti wa Fedha (MA in
Financial Accounting) kutoka Chuo Kikuu cha Dublin City, Jamhuri ya Ireland mwaka 1991.
Profesa Assad pia ana Stashahada ya Kitaaluma ya Uhasibu (Professional Diploma in Accounting) kutoka Chuo Kikuu cha Dublin City mwaka 1990
na Shahada ya Biashara (Bachelor of Commerce) ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam mwaka 1988.
Pamoja na uzoefu wa kitaaluma, Profesa Assad anao uzoefu mkubwa katika eneo la uhasibu na ukaguzi. Alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wahasibu
na Wakaguzi (NBAA) kwa miaka saba (2007 - 2014); ni Rais na Mjumbe wa Chama cha Wahasibu Afrika (Pan African Federation of Accountants) tangu mwaka 2012; na ni mjumbe
wa Bodi kadhaa za Wakurugenzi nchini Tanzania.
Katika kumteua Profesa Mussa Juma ASSAD kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Rais anayo imani kubwa kuwa elimu, weledi, ujuzi na uzoefu ambao Profesa Assad anao
utamwezesha kutekeleza vema majukumu ya nafasi hiyo muhimu sana katika utawala bora wa nchi yetu.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
1 Desemba,2014
Chapisha Maoni