0
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania ametakiwa kutowaonea aibu mawaziri wasiotimiza majukumu yao katika kuwatumikia wananchi
badala yake awachukulie hatua za haraka za kuwawajibisha.

Waumini wa madhehebu mbalimbali ya kikristo nchini Tanzania jana wameungana na wenzao duniani kote kuadhimisha siku kuu ya Krismas
ambayo ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Kwa hapa Tanzania ibada ya kitaifa ilifanyika katika kanisa la pamoja la jumuiya ya Kikristo Chuo Kikuu cha Dar es salaam na kuongozwa na Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya
Zanzibar, Askofu Henry Hafidh. 

Katika mahubiri yake Askofu Hafidh alimtaka Rais Kikwete kutowafumbia macho mawaziri wazembe na wale wasiotimiza majukumu yao katika
kuwatumikia watanzania.

Pia aliwataka waandishi wa Habari nchini kutumia kalamu zao kwa kuandika mambo mema kwa nchi na yenye kuleta tija kwa maendeleo ya taifa
na si kuandika habari ambazo zitavuruga amani ya nchi.

Aliongeza kuwa waandishi ndio wana jukumu la kuwabadilisha wananchi kupenda habari njema kuliko hivi sasa ambapo wanashabikia habari zenye dalili ya kutaka kuvunja amani ya nchi.

Aidha Askofu Hafidh aliwaonya viongozi wa dini kuacha kushabikia masuala ya siasa ambayo inawaingiza kwenye mapambano ya wenyewe na kuacha kufanya kazi ambayo wameagizwa na
mwenyezi mungu juu ya wana damu.

Alisema wanapoona viongozi wa kisiasa
wanakosea, jukumu lao ni kupiga magoti na kuwaombea badala ya kuingilia mambo yasiyowahusu.


Africa Newss

Chapisha Maoni

 
Top