0
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewasili jijini Doha, Qatar jana usiku (Jumamosi, Desemba 20, 2014) kwa ziara ya siku tatu kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo inayotarajiwa kuanza leo.

Lengo la ziara ya Waziri Mkuu ni kukuza
mahusiano baina ya nchi hizi mbili, kuangalia fursa za kiuchumi na miradi mikubwa inayoweza kuzinufaisha nchi hizo na nje ya mipaka yake kwenye Ghuba ya Arabuni (Arabian Gulf) na bara
la Afrika.

Vile vile Waziri Mkuu anatarajiwa kutangaza fursa za uwekezaji nchini Tanzania, fursa za biashara, za utalii na kutafuta mitaji kwa ajili ya sekta za
uchimbaji gesi na mafuta, usindikaji mazao, uvuvi na mifugo, ajira na uendelezaji miundombinu.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Waziri Mkuu atakuwa na mazungumzo ya kiserikali na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Sheikh Abdulla Nasser Al Thani. Vilevile atakutana na Mawaziri wa Kazi na Ustawi wa Jamii; Uchukuzi; Miundombinu na
Uwekezaji wa nchi hii. Naibu Mawaziri
atakaokutana nao ni wa Uchumi na wa Nishati.

Vile vile Waziri Mkuu amepangiwa kukutana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Qatar (Qatar Business Community), wajumbe wa
Chama cha Wafanyabiashara cha Qatar (Chamber of Commerce of the State of Qatar) na pia atakutana na Watanzania waishio Qatar.

Atatembelea pia Mamlaka ya Bandari ya Qatar na makao makuu ya kampuni ya uchimbaji gesi ya Qatar.

Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kimani; Waziri wa Kilimo na Maliasili wa Zanzibar, Dk. Sira Ubwa Mamboya; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Maalim;

Naibu Waziri wa Nishati, Bw. Charles Kitwanga; Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw. Godfrey Zambi.

Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bi. Halima Dendego, wabunge wawili Bi. Amina Makilagi na Bw. Aeshy Hilali na wakuu wa taasisi za TPSF na
TPDC.



IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021, DAR ES SALAAM.
JUMAPILI, DESEMBA 21, 2014

Chapisha Maoni

 
Top