SERIKALI imesema itachukua hatua kali ikiwemo kuwafukuza kazi, kuwavua madaraka, kuwashusha vyeo na kuwakata mishahara viongozi
walioshindwa kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa na kusababisha kasoro na kuvurugika kwa uchaguzi huo katika baadhi ya maeneo nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akitoa taarifa ya awali ya uchaguzi wa Serikali za
Mitaa katika ngazi za Mitaa, Vijiji na Vitongoji uliofanyika juzi.
Alisema taarifa za awali zilionesha kwamba uchaguzi ulikwenda vizuri katika mikoa mingi na kufanikiwa kwa asilimia 98. Lakini, alisema kuna
baadhi ya halmashauri zilikuwa na dosari na kasoro, zilizosababisha baadhi ya maeneo kuahirisha uchaguzi.
“Serikali imepokea kwa uzito taarifa hizi na imesikitishwa sana na vitendo vilivyosababisha uchaguzi huu kuvurugika katika baadhi ya maeneo, hivyo tumeitaka mikoa iwasilishe taarifa
rasmi na kikamilifu kuhusu kilichojitokeza katika halmashauri hizo,” alisema.
Alisema wizara itachambua taarifa hizo ili kubaini wote waliosababisha kasoro ili wachukuliwe hatua kali na stahiki, kulingana na uzito na kiwango cha
uhusika wao, kwa kushindwa kusimamia vizuri uchaguzi na kusababisha kasoro ni moja ya makosa makubwa.
Ghasia aliitaja mikoa ambayo uchaguzi ulikwenda vizuri na ulifanyika katika halmashauri na kata zote kuwa ni Arusha, Mbeya, Kagera, Njombe,
Singida, Lindi, Ruvuma, Katavi, Geita, Iringa, Dodoma na Mtwara.
“Halmashauri ambazo hazina dosari ni 145 kati ya 162 zilizofanya uchaguzi, halmashauri tatu ambazo ni Mkuranga, Kasulu na Kaliua hazikufanya uchaguzi kutokana na vifaa kuchelewa na halmashauri 14 zina kasoro katika
baadhi ya vijiji, vitongoji na mitaa,” alisema.
Aidha, kata zaidi ya 135 hazikufanya uchaguzi, kutokana na kasoro mbalimbali, ambapo uchaguzi
huo utafanyika ndani ya siku saba kama Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa zinavyoelekeza.
Ghasia aliitaja mikoa 13 yenye dosari katika baadhi ya halmashauri na kusababisha kuahirishwa kwa uchaguzi ni Kilimanjaro, Manyara, Morogoro, Shinyanga, Simiyu, Kigoma,
Mwanza, Tabora, Tanga, Mara, Rukwa, Dar es Salaam na Pwani.
Alitaja sababu za kuahirishwa kwa uchaguzi katika halmashauri hizo kuwa ni kucheleweshwa kwa vifaa katika vituo vya kupigia kura, karatasi ya kupigia kura katika nafasi ya mwenyekiti wa kijiji
kuunganishwa na nafasi ya Mwenyekiti wa Kitongoji.
Sababu zingine ni karatasi ya kupigia kura katika sehemu ya nembo ya vyama imechanganywa, ambapo nembo ya chama kingine imewekwa kwa mgombea wa chama tofauti, kuingiliana kwa majina ya wagombea na majina mengine kukosekana kwenye karatasi za kupigia kura na majina ya wagombea kukosewa.
Alisema sababu nyingine ni kukosekana kwa majina ya wajumbe ya wagombea wanaounda serikali katika baadhi ya maeneo, mkanganyiko wa majina ya wagombea wa viti maalumu na karatasi
za kupigia kura kuwa chache ikilinganishwa na Idadi ya wapiga kura.
Alisema katika maeneo mengine uchaguzi haukufanyika, kutokana na karatasi za wapiga kura kuchanganywa na kupelekwa sehemu zisizo sahihi, ambapo karatasi za kata husika zilipelekwa kwenye kata nyingine.
Hata hivyo alisema zipo halmashauri ambazo ziliona dosari mapema na kuzirekebisha. Lakini, alisema zipo ambazo zilirekebishwa, lakini bado
yakarudiwa makosa. Alitaka mikoa na
halmashauri kuwajibika katika kutoa taarifa husika.
Aidha, alisema uchaguzi huo umekuwa na maboresho makubwa tofauti na uliopita wa mwaka 2009. Alisema kwamba wanajipanga uchaguzi
ujao usimamiwe na Tume ya Taifa ya Uchaguziv(NEC).
Alisisitiza kwamba ikionekana uzembe na dosari katika uchaguzi huo, unamhusu yeye, yupo tayari
kuwajibika.
Chapisha Maoni