0
Wakati utata ukizidi kujitokeza katika uapishaji wa viongozi wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Dar es Salaam kutokana na waliodaiwa kushinda kuwekwa kando na kuapishwa walioshindwa,

Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga jana alikumbana na zomeazomea hadi kulazimika kuondoka kwenye Ofisi za Manispaa ya
Ilala, Arnatouglou ambako shughuli hiyo ilikuwa ikifanyika.

Dk Mahanga ambaye pia ni Mbunge wa Segerea (CCM), alizomewa akitakiwa kuondoka katika eneo hilo, akidaiwa kwamba angebadilisha matokeo na
kuwapa ushindi wagombea wa chama chake.

Eneo hilo lilijaa wafuasi wa Chadema, CUF na CCM huku kila kundi likiwa limesindikiza wenyeviti wake kuapishwa katika shughuli ambayo ilifanyika
kwa awamu tatu kwa kila jimbo; Segerea, Ilala na Ukonga kupewa saa mbili.

Waziri Mahanga aliwasili wakati wa zamu ya Segerea saa saba mchana, ndipo kundi la mashabiki wa upinzani lilipoanza kumzomea na kuimba nyimbo za kumkashifu na kutaka atoke
katika ukumbi ulioandaliwa kwa ajili ya
kuwaapisha wenyeviti.

“Escrow... escrow... ondoka, hatukutaki. Hapa hakieleweki mpaka uondoke, hatutaki uchakachuaji wako...” zilisikika sauti za watu mbalimbali huku zikiimba nyimbo mbalimbali kumfukuza mbunge huyo ukumbini.

Baada ya dakika takriban 25 za kelele hizo, waziri huyo alinyanyuka na kuondoka huku wananchi hao wakimsindikiza kwa nyimbo hizohizo na
polisi wakifanya kazi yao ya kuhakikisha
hadhuriki.

Wakati akiondoka, Dk Mahanga alikisogelea kikundi kimoja kilichokuwa kinahoji alichokuwa amefuata wakati shughuli ya uapishaji wenyeviti
haimhusu na kujibu: “Wenyeviti wangu 59 wa Jimbo la Segerea wanaapishwa leo. Kwa nini nisihudhurie? Kelele hizi zinaonyesha jinsi gani ninavyotikisa jiji la Dar es Salaam.”

Baadaye akionekana mwenye kujiamini, mbunge huyo alikatisha katikati ya kundi la mashabiki waliokuwa wakimzomea na kuingia katika gari lake na kuondoka.

Kelele ziliendelea hadi gari la kiongozi huyo lilipotoweka kabisa katika viwanja hivyo.
Walipoulizwa sababu ya kumzomea mbunge huyo, baadhi wa wananchi walisema hawana imani naye
wakidai alichakachua matokeo ya mwaka 2010.

Mmoja wa wananchi hao, Mohamed Said alisema alipofika katika ofisi za halmashauri, dhana iliyomjia kichwani ni uchakachuaji. Aliongeza kuwa kuwapo kwa Dk Mahanga kungesababisha
vurugu kubwa bila sababu.

“Mbona katika maeneo mengine wanakoapishwa wenyeviti wabunge wao hawajaenda, yeye amefuata nini?” alihoji.

Utata wa matokeo
Kama ilivyokuwa juzi katika Manispaa ya Kinondoni ambako ilidaiwa kuwa baadhi ya wagombea walioshinda hawakuitwa kuapishwa lakini wakaitwa wasioshinda, vivyo hivyo katika
Manispaa ya Ilala mambo yalikuwa hayohayo, tofauti ni kuwa hayakurushwa mabomu ya machozi wala risasi.

Jana, madudu zaidi yalibainika katika baadhi ya kata na mitaa, tofauti na juzi, uapishaji uliahirishwa hadi mgogoro uliojitokeza upate
suluhisho.

Baadhi ya majina yaliyoibua utata ni Mariano Maurus, mgombea uenyekiti wa CCM, Mtaa wa Kigogo Fresh B na Ubaya Chuma, aliyekuwa mgombea wa CCM, Mtaa wa Migombani, Kiwalani.

Aliyekuwa mgombea uenyekiti Mtaa wa Kigogo Fresh B kupitia CUF, Patricia Mwamakula alisema uchaguzi katika mtaa huo ulivurugika na mshindi
hakupatikana licha ya kuwa alikuwa amemwacha mbali mpinzani wake.

Alisema siku hiyo fujo zilitokea, masanduku ya kura yakachomwa moto kabla ya matokeo kutangazwa na baadaye walibandikiwa matangazo
kuwa uchaguzi ungerudiwa Jumapili iliyofuata lakini mpaka jana haukuwa umefanyika.

“Tunashangaa kuona mgombea wa CCM anaitwa kula kiapo wakati nilimshinda na hawakutoa matokeo baada ya uchaguzi kuvurugika. Lazima haki itendeke, hatutakubali ufisadi huu,” alisema mama huyo.

Hata hivyo, Maurus ambaye aliitwa jina kula kiapo, alisema ndiye mshindi halali wa Mtaa wa Kigogo Fresh B. Alisisitiza kuwa uchaguzi ulifanyika vizuri na kura zikahesabiwa kabla ya vijana kuanzisha fujo na kuchoma masanduku ya
kura.

“Wakati vurugu zinatokea, wasimamizi walikuwa tayari wamehesabu kura. Masanduku yaliyochomwa moto yalikuwa yamehesabiwa.

Tumezoea kelele za hawa wapinzani, hawana jipya,” alisema Maurus.
Lilipoitwa jina la Mwenyekiti wa Mtaa wa
Migombani – Kiwalani, Chuma watu walianza kupiga kelele kupinga jina hilo. Mwenyekiti huyo alipojitokeza kuingia ukumbini, wananchi walimvuta na kuanza kumpiga.

Hata hivyo, Chuma aliokolewa na askari
waliokuwapo na kupelekwa katika chumba kimoja ili kumnusuru. Alikaa humo muda wote wakati wengine wakiendelea kuapishwa.

Mjumbe wa mtaa huo, Ramadhan Miroba alisema mgombea uenyekiti wa CUF, Kassimu Mshamu alikuwa na nafasi ya ushindi ndiyo maana
wananchi wamepinga jina la huyo mgombea wa CCM.

“Uchaguzi ulivurugika dakika za mwisho kabla matokeo hayajatangazwa, kilichosababisha vurugu siku ya uchaguzi ni masanduku ya kura ya kata
ya Vingunguti kukutwa mtaani kwetu,” alisema mjumbe huyo kupitia CUF.

Utata Pugu Kwalala Katika Mtaa wa Pugu Kwalala, mwenyekiti mteule,
Dorkas Lukiko alishuhudia majina ya watu wasiostahili yakiitwa kuapishwa kama wajumbe wake badala ya wale walioshinda uchaguzi.

“Licha ya mimi kushinda nafasi hii wapo wajumbe watatu wa Chadema na wawili wa CCM lakini nashangaa majina yote yaliyoitwa katika nafasi ya ujumbe ni ya watu wa CCM pekee, tena mmoja
wao ni yule niliyechuana naye katika uenyekiti,” alisema Lukiko na kuongeza kuwa wote wasiostahili hawakuwapo kwa kuwa wanajua kuwa
hawapaswi kuapishwa.

Hata hivyo, baadaye majina hayo yaliyosomwa yalifutwa na wale wajumbe watatu wa Chadema kuapishwa.

Kata tano zawekwa kiporo
Kutokana na utata uliojitokeza katika mitaa hiyo miwili na maeneo mengine, Mwanasheria wa Manispaa ya Ilala, Mashauri Musimu alitangaza
kusimamisha viapo kwa wenyeviti na wajumbe wa kata tano za Jimbo la Segerea kati ya 35.

“Nimeshauriana na mkurugenzi naye ameniambia niwaambie mchague moja kati ya kuendelea na uapishaji wajumbe mliopo au kusitisha mpaka
pale uongozi utakapojiridhisha na wanaostahili.

Kutoapishwa leo hakumaanishi kuwa
hamtambuliki kisheria kwani ninyi ni viongozi halali katika maeneo mtokayo,” alisema Musimu.
Kabla ya kutangaza kuahirisha, Musimu aliwaeleza wafuasi wa vyama waliokuwapo kuwa shughuli hiyo itakamilishwa bila kuhusisha mitaa mitatu yenye utata, jambo lilizua tafrani kwa wafuasi wa Ukawa ambao waliwataka viongozi wao
wasishiriki.

“Taarifa zilizopo ni kwamba katika Mtaa wa Segerea -Migombani uchaguzi haukufanyika na watapangiwa tarehe ya kurudia wakati Kigogo Fresh B wamekuja watu wawili. Kiwalani -
Migombani ni haya mnayoyakataa, yote haya yanahitaji kujiridhisha kabla hatujayatolea uamuzi ingawa tunaweza tukaendelea na wale waliopo,”
alisema Musimu.

Baada ya kauli hiyo wafuasi wa Ukawa
walisimama na kutaka kutoka nje ya ukumbi lakini polisi waliwashawishi wabaki ndani kupata suluhu
ili kuepusha vurugu ambazo zingeweza kutokea.

Hali ya ulinzi Kutokana na umati uliokuwapo, polisi walisoma
mchezo na kuandaa utaratibu wa kuita majina ya wajumbe wote waliotakiwa kuingia katika ukumbi huo, tofauti na hali ilivyokuwa juzi Kinondoni.

Kilichokuwa kinafanyika ni kuita jina la mwenyekiti wa mtaa husika ambaye alitakiwa kuwatambua wajumbe wake ili waingie ndani.

Kutokana na udogo wa ukumbi, wajumbe hao walilazimika kuingia kwa awamu kulingana na majimbo yao na ilipofika zamu ya Segerea kwa
wingi wa mitaa yake nao walilazimika kuingia kata moja baada ya nyingine.

Shughuli hiyo ilifanyika kwa mafanikio katika awamu mbili za kwanza lakini ilipata kikwazo katika awamu ya tatu baada ya kelele nyingi za wafuasi wa Ukawa kushinikiza isitishwe mpaka
pale dosari zitakaporekebishwa.

Kata tano ziliathirika na usitishaji huo ambazo ni Kimanga, Kisukuru, Liwiti, Kinyerezi pamoja na Segerea kutokana na utata uliojitokeza katika mitaa mitatu ya Kiwalani - Migombani, Segerea -
Migombani na Kigogo Fresh B ambako kulikuwa na utata wa matokeo.

Baada ya kusitishwa, wafuasi wa Ukawa
waliokuwa wamewasindikiza wagombea wao walishangilia na kuimba nyimbo za kujipongeza kwa kufanikisha kile walichokiita kuzuia unyongaji
wa demokrasia.

Chapisha Maoni

 
Top