Mabao ya Mbwana Samatta na Shiza Kichuya yalitosha kuwapa furaha Watanzania baada ya timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kuichapa Congo mabao 2-0
Katika mchezo huo wa kirafiki uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam,Taifa Stars ilicheza vizuri muda mwingi wa mchezo na kuwapa wakati mgumu wapinzani wao ambao walijaza wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa barani Ulaya.
Taifa Stars iliyochapwa mabao 4-1 na Algeria katika mchezo mwingine wa kirafiki uliofanyika wiki iliyopita, leo Jumanne ilionekana kubadilika na kuusaka ushindi kwa nguvu huku ikipewa sapoti kubwa na mamia ya mashabiki waliofurika uwajani hapo.
Timu zote zilianza mchezo kwa kasi na kushambuliana kwa zamu, lakini mabeki wa pande zote mbili walikuwa imara kuokoa hatari mbalimbali langoni mwao.
Samatta aliwainua mashabiki waliofurika uwanjani hapo dakika 74, akiunganisha kwa kichwa krosi safi iliyopigwa na Shiza Kichuya.
Bao hilo lilionekana kuwaamsha Stars na kuzidi kulishambulia lango la Congo kama nyuki na hivyo kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 86 kupitia kwa Kichuya
aliyemalizia pasi safi ya Samatta.
Ushindi huo unaweza kuipandisha Taifa Stars katika viwango vya ubora wa soka vinavyotolewa na Shirikisho la soka Duniani(Fifa).
Taifa Stars na DR Congo wamekutana mara sita tangu 1995, mara mbili katika mechi za mashindano na mara nne katika michezo ya kirafiki.
Tanzania imeshinda mechi mara tatu, sare moja na kufungwa mechi mbili mara ya mwisho zilipokutana Februari 23, 2012 timu hizo zilitoka suluhu.
Chapisha Maoni