0
TIMU ya Taifa chini ya miaka 17 'Serengeti Boys' haijawaangusha umati wa mashabiki waliojitokeza kuangalia mechi yao dhidi ya Sudan.
Katika kipindi cha kwanza timu zote zilikuwa zikicheza kandanda safi kwa utulivu wa hali ya juu katika kupiga pasi za uhakika.
Serengeti walipata bao lao la kwanza kupitia kwa Edson Mshirakandiambaye alipiga kona ya moja kwa moja na kumshinda kipa wa Sudan, Omer Miso baada ya kumponyoka mikononi.
Bao hilo liliamsha hisia kwa mashabiki waliojitokeza katika uwanja wa Taifa lakini bado vijana wa Serengeti walionyesha kusaka mabao ya ziada kwa kutengeneza nafasi kadhaa.
Katika kipindi cha pili Serengeti walianza kwa kushambulia kwa mfululizo na walipata bao la pili dakika 48 kupitia kwa Kelvin John aliyeunganisha pasi ya Morice Abraham.
Dakika 55 Serengeti walipata penalti baada ya beki wa Sudan kuunawa mpira, lakini hata hivyo mchezaji Salum Lupepo alikosa penalti hiyo na kumfanya kipa Omer Miso kuudaka mpira huo bila tabu.
Sudan nao walionekana kujipanga upya kwa kucheza soka la utulivu, lakini hata hivyo walikuwa na kazi kubwa katika kupenya kwenye safu ya ulinzi ya Tanzania.
Dakika 60 Serengeti walianzisha mashambulizi kutoka nyuma, kiungo Moses Abraham alipiga mpira mrefu akiwa katikati ya uwanja na kukutana na Kelvin John aliyefunga bao la tatu katika mchezo huo huku yeye akiwa amefunga bao la pili katika mechi hiyo.
Sudan walionekana kuzidiwa mbinu za ufundi kwani walianza kukaba kuliko kushambulia na dakika 75 Agiri Ngoda, aliifungia Serengeti bao la nne baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Sudan.
Dakika 80 Serengeti walipata bao la tano baada ya Ladaki Chasambi kupiga krosi upande wa kulia na kumaliziwa vizuri na Salum Milinge.
Hata hivyo Serengeti Boys iliziona nyavu za Sudan mara kumi hata hivyo mabao 5 yalikataliwa baada ya mwamuzi kuamuru yalikuwa ya kuotea.

Chapisha Maoni

 
Top