Real Madrid walianza maisha bila mshambuliaji wao nyota wa zamani Cristiano Ronaldo na meneja Zinedine Zidane kwa kushindwa 4-2 katika debi ya kombe la Super Cup ya Uefa na wapinzani wao wa jadi Atletico Madrid.
Mabao mawili ya muda wa ziada kutoka kwa Koke na Saul yaliwasaidia Atletico kushinda mechi hiyo iliyokuwa imemalizika 2-2 katika muda wa kawaida.
Ilikuwa mechi yao ya kwanza ya ushindani tangu Ronaldo alipohamia Juventus ya Italia kwa £99m majira ya joto na pia baada ya kuondoka kwa Zidane ambaye nafasi yake ilichukuliwa na aliyekuwa meneja wa timu ya taifa ya Uhispania Julen Lopetegui.
Atletico walishinda Super Cup kwa mara yao ya tatu na kuhakikisha kwamba hawajawahi kushindwa katika mechi za Super Cup kwani wameshiriki mara tatu.
Nyota wa zamani wa Chelsea Diego Costa alikuwa amewafungia Atletico mabao mawili muda wa kawaida, la kwanza sekunde 49 baada ya mechi kuanza na la pili kipindi cha pili.
Gareth Bale alikuwa amemuwezesha Karim Benzema kufunga bao la kwanza la Real kwa kichwa kabla ya nahodha wao Sergio Ramos kufunga penalti na kuwaweka kifua mbele 2-1 kwa muda baada ya Juanfran kuadhibiwa kwa kunawa mpira eneo la hatari.
Beki kamili Marcelo alipoteza nafasi ya kuwafungia Real bao la ushindi sekunde za mwisho za muda wa kawaida mechi hiyo, na kuwapotezea mabingwa hao wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya nafasi ya kuwa klabu ya kwanza ya kushinda kombe hilo mara tatu mtawalia.
Mwaka jana, Real waliibuka washindi kwa kuwalaza Manchester United 2-1 na mwaka uliotangulia walikuwa wamewalaza Sevilla 3-2.
Ilikuwa ni mara ya nne katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kwa Super Cup ya Uefa kushindaniwa na klabu mbili za Uhispania, lakini mara ya kwanza kwa klabu kutoka jiji moja kukutana.
Maisha bila Ronaldo
Real Madrid walipokuwa wanaonekana kutatizika kuyazoea maisha bila Ronaldo, Atletico ndio walioonyesha ustadi wa hali ya juu.
Hali kwamba Real hawakumnunua mchezaji anayeonekana kutazamiwa kujaza moja kwa moja pengo lililoachwa na Ronaldo inawatia wasiwasi mashabiki wa Real lakini bado kuna washambuliaji wenye uzoefu mkubwa.
Marco Asensio na Bale ni wachezaji wawili ambao watatumai kufaidi kutokana na kuondoka kwa Ronaldo.
Takwimu muhimu
Atletico Madrid ndio walishindi wa kwanza wa Europa League walioshinda Uefa Super Cup tangu walipofanya hivyo dhidi ya Chelsea mwaka 2012.
Real Madrid walifungwa mabao manne na zaidi katika mechi kwa mara ya kwanza tangu Novemba 2015 dhidi ya Barcelona katika La Liga wakiwa chini ya Rafael Benitez - hawakuwahi kufungwa hivyo chini ya Zidane.
Lopetegui ndiye meneja wa kwanza wa Real Madrid kufungwa maba manne au zaidi katika mechi yake ya kwanza ya ushindani na klabu hiyo tangu Michael Keeping dhidi ya Celta Vigo mnamo Februari1948.
Bao la Costa la Atletico Madrid sekunde ya 49 ndilo la kasi zaidi kuwahi kufungwa katika mechi ya UEFA Super Cup.
Alifungia klabu hiyo mabao mawili mechi moja kwa mara ya kwanza tangu kurejea Atletico Madrid, mwisho alifanya hivyo akiwa na Chelsea dhidi ya Southampton katika Ligi ya Premia mnamo Aprili 2017.
Karim Benzema alifunga dhidi ya Atletico Madrid kwa mara ya kwanza tangu Oktoba 2015 katika mechi ya La Liga - alikuwa amekwenda mechi nane bila kuwafunga.
Ramos sasa amefunga mabao matano dhidi ya Atletico Madrid - ni dhidi ya Sevilla pekee Ramos (sita) amefungia Real Madrid mabao mengi zaidi. Mabao yote mawili ameyafunga katika michuano ya kushindania vikombe.
Chapisha Maoni