0
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye, amewataka wananchi wasikubali kuandamana kwa shinikizo la viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ili kushinikiza Bunge Maalumu la Katiba lisitishe
vikao vyake kabla ya Oktoba 4,2014.

Bw. Nnauye aliyasema hayo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Wilaya ya Kisarawe,
mkoani Pwani na kusisitiza kuwa, maandamano hayo aachiwe Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Bw. Freeman Mbowe, familia yake na viongozi
wengine.

Alisema chama hicho kina utamaduni wa kutumia damu za Watanzania kama mtaji wake kisiasa
kwani vyombo vya dola vinapochukua hatua ya kuzuia maandamano, wanaoathirika si viongozi wa
chama hicho au familia zao ndio maana wanaona fahari watu wanapokufa.

"Upinzani katika nchi hii umegeuka kuwa laana, kazi kubwa ambayo wanaifanya ni kuchonganisha watu na Watanzania ni mashahidi, maeneo ambayo CHADEMA wamefanya maandamano, watu
maskini wamepoteza maisha.
"Viongozi wa CHADEMA wanabaki salama na familia zao hivyo kama Mbowe anataka kufanya maandamano nchi nzima kushinikiza Bunge la
Katiba lisitishwe, aanze kutangulia yeye, mkewe na watoto wake , Watanzania wamechoka kushuhudia damu za watu maskini zikimwagika,"alisema Nape.

Aliwataka wananchi kufahamu kuwa, Katiba haimpeleki mwanasiasa au mtu yoyote Ikulu badala yake kura ndizo zinazoweza kumpeleka
Ikulu ambapo CHADEMA, Chama cha Wananchi (CUF) pamoja na NCCR-Mageuzi, wanaamini Katiba ikipatikana ndio inayoweza kuwapa ushindi
katika Uchaguzi Mkuu 2015.

"Vyama hivi vinataka kuligawa Taifa kwa kutumia mchakato wa Katiba, umefika wakati wa Watanzania kuachana na upinzani wenye kujenga chuki...CCM na viongozi wake wamekuwa wakihubiri amani, mshikamano na umoja lakini
wapinzani wanatumia muda mwingi kuhubiri chuki," alisema.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Abdulrahman Kinana, amepongeza juhudi za Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete, kwa
juhudi zake za kuwasaidia wanawake na watoto wa kike kupitia taasisi hiyo.
Bw. Kinana alitoa pongezi hizo juzi baada ya kutembelea Shule ya Wanawake ya Wama Nakayama, inayomilikiwa na taasisi hiyo iliyopo
kwenye Kijiji cha Nyamisati, Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani.

Alisema Mama Kikwete amekuwa na mchango mkubwa nchini kutokana na jitihada zake za kusaidia makundi mbalimbali wakiwemo watoto
yatima na waishio katika mazingira magumu.

Aliwataka wanafunzi shuleni hapo, kusoma kwa bidii ili kuunga mkono juhudi za Mama Kikwete kwani wao ndio viongozi wa baadaye ambao
watashika nafasi mbalimbali za uongozi.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Suma Mensah, alisema shule hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa Rufiji na nje ya
Wilaya hiyo kwani inatoa elimu kwa wanafunzi wasio na uwezo pamoja na yatima.

"Juhudi za Mama Kikwete kwa watoto wa kike zimefanikiwa kwani watoto waliokuwa hawana mwelekeo wa maisha, hivi sasa wanafurahia kupata elimu bora, " alisema Mensah.

Chapisha Maoni

 
Top