0
Rais Jakaya Kikwete ametoka wodini katika Hospitali ya Johns Hopkins na kuhamishiwa kwenye hoteli maalumu ambako ataendelea kuwa
chini ya uangalizi wa madaktari.

Rais Kikwete alifanyiwa upasuaji wa tezi dume wiki iliyopita na afya yake imekuwa ikiimarika siku hadi siku.

Makundi mbalimbali ya wananchi yamekuwa yakimtakia uponaji wa haraka kwa njia ya ujumbe
mfupi wa simu.
Miongoni mwa waliomtakia afya njema ni familia ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambayo imeeleza kupokea kwa masikitiko taarifa za
kuugua kwake na kumwombea apone haraka ili aendelee na majukumu yake kwa Taifa.

Chama cha RPP cha Rwanda kimemtumia salamu za pole Rais Kikwete na kuungana na mamilioni
ya Watanzania kumwombea ili arejee katika afya yake na majukumu ya kila siku.
“RPP tutashirikiana na familia, marafiki na mamilioni ya Watanzania kumwombea Rais Kikwete aweze kupona haraka. Rais Kikwete ni
jirani yetu na mtetezi mkubwa wa kanda hii katika kupata ukombozi wa kijamii, kisiasa na kiuchumi,” ilisema taarifa ya RPP kwa umma iliyotolewa na
Rais wa chama hicho, John V Karuranga.

Aondoka wodini Wakati Rais Kikwete akiondoka wodini, alikuwa
anatembea akiwa amesindikizwa na daktari bingwa, Edward Schaeffer kutoka Hospitali ya Johns Hopkins na mkewe Salma.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu iliyotolewa juzi ilisema: “Afya yake imekuwa inaimarika kiasi cha kuanza mazoezi ya kutembea
na akiwa katika hoteli hiyo, ataendelea kuwa chini ya uangalizi wa madaktari.”
Iliongeza: “Rais Kikwete ataendelea kupatiwa matibabu, kutembelewa mara kwa mara na madaktari na kuwa chini ya uangalizi wa wauguzi muda wote. 


Wiki moja baadaye, Rais Kikwete
atafanyiwa tathmini ya kuwawezesha madaktari kuamua hatua inayofuata ya matibabu yake.” Taarifa hiyo ilisema: “Kutokana na kuondolewa kwa bandeji kwenye mshono ambao nao umeanza
kukauka vizuri, Rais Kikwete atakuwa katika hoteli maalumu (haikutajwa), iliyo na uhusiano na Hospitali ya Johns Hopkins.”

Chapisha Maoni

 
Top