0
MMOJA wa madereva waliosababisha ajali ya mabasi ya City Boy Jumatatu iliyopita katika kijiji
cha Maweni wilayani Manyoni, Jeremiah
Semfungwe (34), amefikishwa katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Singida akikabiliwa na makosa 30 ya kuua bila kukusudia.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Joyce Minde, ilidaiwa kuwa
mshitakiwa Semfungwe alitenda makosa hayo
Julai 4 mwaka huu saa 8.15 mchana wakati akiendesha basi T. 247 BCD mali ya Kampuni ya
City Boy kwa kuligonganisha na basi T.331DCE.
Wakili Mkuu Mfawidhi wa Serikali, Zakaria Ndaskoi
alidai kuwa siku ya tukio mshitakiwa ambaye ni
dereva na mkazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam, bila kukusudia, alisababisha vifo vya abiria 30 kinyume na Kifungu 195 na 198 cha
Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Toleo la Kwanza.
Wakili wa mshitakiwa, Francis Kitope aliiomba
mahakama impe mteja wake dhamana kwa kuwa
chini ya Kifungu 148 cha Mwenendo wa Makosa
ya Jinai, kosa hilo linadhaminika.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Ndaskoi alipinga
hoja hiyo kwa kudai kuwa kwa kufanya hivyo
usalama wa mshitakiwa utakuwa hatarini kwa
kuwa ndugu wa marehemu na majeruhi bado
wana hasira kutokana na ajali hiyo kuwa bado
“mbichi”.
Aidha, Ndaskoi ambaye alikuwa akisaidiana na
Petrida Muta aliendelea kudai kuwa majeruhi 54
wa ajali hiyo hali zao bado ni mbaya na hatma
yao haijulikani hivyo si vyema mshitakiwa
kupewa dhamana na kwamba mshitakiwa
mwingine, dereva Boniface Mwakalukwa
ametoroka.
Mshitakiwa hakutakiwa kujibu lolote kutokana na
mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka juu ya
kesi za mauji na ameswekwa rumande hadi Julai
21 kesi yake itakapotajwa tena.

Chapisha Maoni

 
Top