HUZUNI imetanda katika wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, baada ya ajali ya moto wa kibatari kuteketeza watoto wanne wa mama
mmoja, waliokuwa wamefungiwa chumbani na dada anayewalea.
Ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana katika mtaa wa Nyerere, mji mdogo wa Kibaigwa wilayani Kongwa, wakati mama wa watoto hao
aliposafiri kwenda shambani Kiteto mkoani
Manyara, kwa ajili ya kuvuna mazao na kuwaacha
watoto wake mikononi mwa dada, aliyekuwa
akimsaidia kuwalea.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Lazaro
Mambosasa alisema chanzo cha ajali hiyo ni
mlipuko wa kibatari kilichokuwa ndani ya chumba
walicholala watoto hao, ambacho kilichoma
godoro na kuteketeza nyumba yote.
Moto huo ulioanzia katika chumba hicho,
umeelezwa kuteketeza nyumba yote ya vyumba
sita iliyojengwa kwa tofali za udongo mali ya
Nelson Mdachi.
Kamanda Mambosasa aliwataja watoto hao kuwa
ni Elizabeth Nelson (11) mwanafunzi wa darasa la
saba, Samweli Mdachi (7) anayesoma darasa la
kwanza na Nase Mgomba (9) anayesoma darasa
la pili katika shule ya msingi Miembeni na Peter
Lema (9) mwanafunzi darasa la tatu shule ya
msingi St Paulo.
Kutokana na ajali hiyo, Kamanda Mambosasa
amewakumbusha wazazi wasiache watoto peke
yao nyumbani kwa kuwa ni hatari kwani ajali
ikitokea ni vigumu kuokolewa.
Taarifa kutoka kwa watu wa karibu na majirani wa
familia hiyo, zimedai kuwa mama wa familia hiyo
alikwenda shambani kuvuna mazao katika wilaya
ya Kiteto, mkoani Manyara na kuwaacha watoto
hao chini ya uangalizi wa msichana aliyefahamika
kwa jina moja la Ester.
Kwa mujibu wa madai yao, ilipofika usiku Ester
anayetajwa kuwa na jukumu la kulea watoto hao,
alitoka na kwenda kusikojulikana huku
akiwafungia watoto hao kwa nje.
Mkazi wa Kibaigwa, Denis Luhunga,
alipozungumza na mwandishi kuhusu ajali hiyo
alidai kuwa kibatari kilipolipuka, kilisababisha
godoro kushika moto na kuteketea kwa watoto
hao.
“Aliwafungia watoto ndani akaacha kibatari
kinawaka, baada ya kulipuka moshi mwingi ulijaa
ndani,” alidai Luhunga.
Kuhusu alipo baba wa familia hiyo, mkazi
mwingine wa eneo la tukio hilo, Paulo Sauli
alisema baba wa watoto hao, aliyemtaja kwa jina
la Nelson Mdachi, alishakufa miaka mitatu
iliyopita na jukumu la kuwalea aliachiwa mama
yao.
Alifafanua kuwa baba huyo ambaye wakati wa
uhai wake alifahamika kwa jina maarufu la ‘Moja
kwa moja’, alikufa baada ya kuanguka kutoka juu
ya mti alipokuwa akirina asali na tangu hapo,
jukumu la kulea likabaki kwa mama mzazi wa
watoto hao.
“Tukio hilo limetusikitisha sana ni tukio baya
maana wameteketea kabisa hajulikani nani ni
nani,” alisema Sauli na kuongeza, “Hata Ester
hafahamiki alipo, kuna watu wengi lakini
tumemuangalia hapa msibani hatumuoni.”
Taarifa nyingine kutoka eneo la tukio, zilidai kuwa
Mdachi alizaa na mama huyo watoto wawili na
baada ya kufariki, mama huyo alizaa watoto
wengine wawili na wanaume wengine.
Chapisha Maoni