0
Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye shughuli za utalii iliyoanza mwezi huu, imezishtua nchi 30 za Ulaya ambazo zimeiandikia
barua Serikali ya Tanzania zikiomba ifikirie upya
au isianze kutumika hadi mwaka ujao.
Kodi hiyo, ambayo ni sehemu ya mkakati wa
Serikali kukusanya mapato ili kuondokana na
utegemezi, ilitangazwa kwenye Bunge la Bajeti
lililopita na tayari Sheria ya Fedha imeshapitishwa
kubariki matumizi yake, licha ya wabunge
kuipinga kwa maelezo kuwa itazipa nchi
washindani mwanya wa kukuza utalii.
Dk Philip Mpango alisema walipata wazo la
kuanzisha kodi hiyo kutoka nchi jirani ya Kenya,
lakini wakati akitangaza hayo waziri mwenzake
wa nchi hiyo alitangaza kuiondoa baada ya utalii
kuathirika kutokana na mashambulizi ya kigaidi.
Wakati sheria hiyo ikianza kutumika nchini, nchi
hizo za Ulaya ambazo ni wadau wakuu katika
sekta ya utalii zimemwandikia barua hiyo Dk
Mpango, naibu wake, Dk Ashatu Kijaji na Waziri
wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne
Maghembe.
Chama cha Kitaifa wa Mawakala wa Usafiri na
Wasimamizi wa Utalii (ECTAA) kutoka nchi 30 za
Ulaya ndicho kinachoziwakilisha kampuni zaidi ya
70,000 za utalii barani humo. Nchi hizo ndizo
zinazotoa asilimia 50 ya watalii wote duniani.
Katika barua yao iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa
ECTAA, Michel de Blust, nchi hizo zilieleza
wasiwasi wao kutokana na utambulishwaji wa
ghafla wa kodi hiyo katika huduma za utalii,
zikisema uamuzi huo unaongeza gharama za
safari nchini.
“Najua utakubaliana na mimi kuwa kodi ina
umuhimu wake na ina madhumuni yake, lakini
inaweza kubadili mawazo ya watalii na
wakachagua maeneo mengine,” inasema barua ya
Blust.
Waziri wa Fedha na Mipango, “Mfano mzuri ni
Kenya, utambulishaji wa kodi katika huduma za
utalii mwaka jana ulishusha idadi ya watalii kwa
asilimia nne na baadaye Kenya waliamua
kuachana na kodi hiyo ili kudumisha ushindani
wake.”
Barua hiyo inasema kodi hiyo katika huduma za
utalii itaathiri waandaaji wa safari za watalii
wanaotoa huduma nchini kwa sababu hakukuwa
na tangazo la kuwaandaa kabla ya kuanzishwa
kwa tozo hiyo.
“Waandaaji wa safari wa Ulaya wanawajibika na
sheria inayomlinda mteja, hivyo wanatakiwa wawe
wanafahamu bei na kodi mpya kabla. Kwa sasa ni
vigumu mno kwa waandaji kubadili bei zao
ghafla,” inasema barua hiyo.
Kadhalika, barua hiyo inaeleza kuwa Wakala wa
Utalii wa Tanzania uliwasiliana na Wakala wa
Ulaya kuhusu kodi hiyo na mawakala wa Ulaya
wanatafakari kama wanaweza kuingia gharama
hiyo au kujiondoa katika mpango huo.
“ Kama kodi hii ikiahirishwa, basi waandaaji wa
safari za watalii watajipanga kuingia gharama hizi
na kubadili mfumo wote wa huduma hizo Ulaya,”
inasema barua hiyo.
Hivi karibuni, Waziri Maghembe alinukuliwa
kwenye mkutano wa Shirika la Hifadhi za Taifa
(Tanapa), akisema kuwa Serikali haitabadili
msimamo huo.
Alisema Sh7 bilioni wanazotarajia kupata kwa
kutoza VAT kwenye huduma za utalii, zitawapa
uwezo wa kutangaza utalii nje ya nchi na kuziba
pengo la bajeti linalotokana na kushuka kwa utalii
wa uwindaji. Alisema VAT itakayokatwa ni asilimia
18 ya kitu kilichonunuliwa na inatozwa wakati wa
kununua huduma ya utalii.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja
Jenerali Gaudence Milanzi alisema hajaiona barua
ya ECTAA, lakini akasema watafanya kikao na
Chama cha Wafanyabiashara za Utalii Tanzania
(Tato) ili kujadili nini kifanyike ili sekta ya utalii
isiyumbe.
“Hili ni suala mtambuka na hii VAT ilipitishwa na
kikao cha bajeti, wizara kwa sasa haina la kufanya
zaidi ya kutafuta njia mbadala ili sekta isiyumbe,”
alisema.
Tovuti kwa ajili ya watalii ya Afrika,
Safaribookings.com imeeleza kuwa wamekuwa
wakipata barua pepe kutoka kwa wateja ambao
wamepewa taarifa kutoka kwa wasimamizi wa
watalii kulipa fedha za ziada.
Marc Harris, mkurugenzi wa kampuni ya Tanzania
Odyssey inayotoa huduma za kitalii na yenye
makazi yake nchini, aliliambia gazeti la Daily
Telegraph la Uingereza kuwa kodi mpya ni janga
kubwa ambalo halikutarajiwa na wengi.
“Watanzania wanaweza kufanya chochote kuhusu
kodi, lakini suala la muda ndiyo tatizo. Wametupa
taarifa hizi Juni 23, wiki moja tu kabla ya kodi
kuanza kutozwa,” alikaririwa na gazeti hilo.
Alisema gharama kubwa itaonekana kwenye
malazi ambayo inaonekana kuongezeka kwa
asilimia saba.
“Kinachoshangaza ni kuwa Hifadhi za Taifa
hazijasajiliwa VAT, lakini inatoza fedha hizo. Sijui
watazitumiaje,” alisema Harris.
Mmiliki wa kampuni ya kitalii ya
Safaribooking.com, Wouter Vergeer alisema muda
mfupi waliopewa umewashtua.
“Maelfu ya wateja wameshtushwa na chaji hizo
ambazo hazikutarajiwa. Wengi hawajapata muda
wa kujipanga kwa tozo hizo, hata risiti zenyewe
za VAT hatuna,” alisema.

Chapisha Maoni

 
Top