0
Mashirika yanayotetea haki za wanawake na
usawa wa kijinsi nchini yamesema uteuzi wa
nafasi muhimu za uongozi serikalini unaofanywa
na Rais John Magufuli, hauzingatii hali halisi ya
uwakilishi wa kijinsia.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kwa niaba
ya mashirika hayo, Mkurugenzi wa Mtandao wa
Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi alisema licha
ya kupiga kelele tangu uteuzi wa Baraza la
Mawaziri kuwa haukuzingatia usawa huo, bado
hali inaonekana kuwa tete kwa upande wa
wanawake.
Alisema katika baraza hilo, kati ya mawaziri 19,
wanne pekee ndiyo wanawake sawa na asilimia
21.1 ya mawaziri wote ikilinganishwa na uteuzi
wa baraza la Serikali ya Awamu ya Nne ambalo
lilikuwa na mawaziri wanawake 10 sawa na
asilimia 33.3.
Alisema manaibu waziri kati ya 16 waliopo,
wanawake ni watano sawa na asilimia 31.25.
“Ukiangalia upande wa makatibu wakuu,
walioteuliwa ni 29 kati ya hao, wanaume ni 26
sawa na asilimia 89.7 huku wanawake
wakipungua kutoka watano sawa na asilimia 21.7
ya mwaka 2014 hadi kufikia watatu sawa na
asilimia 10.3 kwa sasa,” alisema Liundi.
Alisema uteuzi wa wanawake katika nafasi hizo
umepungua kwa asilimia 10. Katika nafasi ya
wakuu wa mikoa, Liundi alisema idadi ya
wanawake imeshuka zaidi, kati ya wakuu wa
mikoa 26 Tanzania Bara, 21 ni wanaume sawa na
asilimia 80 na wanawake ni watano sawa na
asilimia mbili.
Kadhalika, alisema idadi ya wakuu wa wilaya
imezidi kuporomoka ikilinganishwa na ya Februari
mwaka jana ambako wanawake walikuwa asilimia
35.07: “Kwa maana nyingine, hapa uteuzi
umepungua kwa asilimia saba.”
Liundi alisema mikoa mitatu ya Simiyu, Songwe
na Singida haina wawakilishi wanawake kwa
nafasi ya ukuu wa wilaya.
“Hii iko hata kwenye nafasi za makatibu tawala
wa mikoa na wilaya na wakurugenzi wa
halmashauri, hatuoni idadi ya wanawake
ikiongezeka na badala yake inashuka,” alisema.
Mwakilishi wa Taasisi ya Women Fund Tanzania
(WFT), Dk Dinna Mbaga alisema Tanzania ni kati
ya mataifa duniani yaliyoridhia na kusaini
mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda
inayoweka misingi ya usawa kwa binadamu
ikiwamo ushiriki katika ngazi zote za uamuzi,
lakini haitekelezi mikataba hiyo kwa ridhaa mpaka
isukumwe na asasi za kiraia jambo linaloleta
ukakasi.
Alisema miongoni mwa mikataba hiyo ni Tamko
la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu (UDHR:
1948), Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza aina
zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW:
1979), Mpango kazi wa Beijing (1995), Mkataba
wa Ziada wa Maputo na Mkataba wa Nyongeza wa
Jinsia na Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Mwakilishi wa Chama cha Waandishi wa Habari
Wanawake Tanzania (Tamwa), Gladness Munuo
alisema Tanzania kupitia Dira ya Maendeleo ya
2025, imetambua kuwa mojawapo ya vichocheo
vya ukuaji wa uchumi ni pamoja na kuwa na jamii
yenye maono ya kimaendeleo na utamaduni
wezeshi kwa wanawake na makundi mengine.

Chapisha Maoni

 
Top