0
JESHI la Polisi mkoani Dodoma linawashikilia
viongozi watatu wa Baraza la Vijana la Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) Taifa,
kwa uchochezi na kuikashifu serikali.
Pia viongozi hao wanadaiwa kuvaa fulana zenye
maandishi demokrasia imenyongwa, huku
nyingine zikiandikwa dikteta uchwara.
Wanaoshikiliwa ni pamoja na Mwenyekiti wa
Bavicha- Taifa, Patrobas Katambi, Katibu wa
Bavicha-Taifa, Julius Mwita na Mwenyekiti wa
Bavicha mkoani Mbeya, George Tito.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro
Mambosasa alisema watuhumiwa hao
watashikiliwa mpaka Jumatatu watakapofikishwa
mahakamani.
“Hawatadhaminiwa mpaka Jumatatu,
watakapofikishwa mahakamani,” alisema.
Kamanda Mambosasa alisema kitendo cha
viongozi hao kuvaa fulana inayosema demokrasia
imenyongwa, inamaanisha serikali inanyonga
demokrasia, jambo ambalo ni la uchochezi.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelezea
tukio hilo Mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema-
Taifa, Joseph Kasambala alidai walikuwa katika
ziara katika baadhi ya mikoa, wakianzia mkoani
Mara katika Kijiji cha Mwitongo, Mwanza kabla
hawajafika Dodoma juzi saa 8:00 mchana.
Alisema jana walikusudia kukutana na vyombo
vya habari mjini Dodoma kuelezea hatua
iliyofikiwa katika mpango wao wa Bavicha – Taifa
kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoani Dodoma,
kuzuia wanachama wa CCM kufanya Mkutano
Mkuu wa Taifa, Julai 23 mwaka huu.
Alidai wakiwa katika baa ya Cape Town, usiku
aliwaacha wenzake na kwenda kukutana na jamaa
yake mwingine na baadaye alipata taarifa za
wenzake kukamatwa na polisi.
Kwa mujibu wa madai ya Kasambala,
kilichomsikitisha ni kukataliwa kuonana nao
alipofika kwenye kituo kikuu cha polisi jana
asubuhi ambapo alitakiwa kwanza akaonane na
viongozi wa Polisi wa wilaya na mkoa (OCD,
RPC).
Kasambala alidai taarifa alizopatiwa kwenye kituo
hicho cha polisi, zilieleza kuwa kosa
wanalotuhumiwa kufanya ni kukashifu serikali,
kwa kuvaa fulana yenye maandishi ‘Dikteta
Uchwara’, tuhuma alizodai kuwa si za kweli.
Alionesha fulana aliyokuwa amevaa, yenye rangi
nyeusi na maandiko meupe yanayosema, ‘Mwl.
Nyerere: Demokrasia inanyongwa’ upande wa
mbele ikiwa na maandishi ‘haki na amani’.
Alidai kuwa ziara yao inajumuisha viongozi sita
wa Bavicha, akiwemo yeye, watatu waliokamatwa
ambao ni Katibu Mwenezi wa Bavicha – Taifa,
Edward Simbeye na Katibu wa Bavichamkoani
Temeke, Hilda Newton.
Kasambala alidai kuwa baada ya kikao hicho,
wangerejea Dar es Salaam, ili kukamilisha
mikakati hiyo akisema ingawa wanafahamu kuwa
hawana mamlaka ya kuzuia mkutano huo wa
CCM, lakini wanao wajibu wa kushirikiana na
polisi kama raia wema, kuhakikisha maagizo ya
serikali yanazingatiwa.
Hivi karibuni, viongozi wa BAVICHA wakiwa jijini
Dar es Salaam, walitangaza msimamo wao wa
kuzuia mkutano huo kwa kutumia wanachama
wake wapatao 4,000.
Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick ole
Sosopi, alidai kuwa vijana hao watatoka sehemu
mbalimbali ili kuzuia mkutano huo wa CCM ili
kusaidia Jeshi la Polisi kutekeleza amri yake ya
kuzuia mikutano ya kisiasa hadi 2020.


Chz
Mpekuzi

Chapisha Maoni

 
Top