0
Kwa mujibu wa gazeti la Champion, Simba
imeamua kutegua kitendawili na kukiri kuwa
msimu ujao hawatakuwa na mshambuliaji Mganda,
Hamis Kiiza na tayari wamemalizana kwa amani.
Tangu kumalizika kwa Ligi Kuu Bara 2015-16,
kumekuwa na taarifa mbalimbali juu ya kutemwa
kwa mshambuliaji huyo kutokana na sababu za
utovu wa nidhamu lakini hakukuwa na kiongozi
aliyewahi kuthibitisha kuhusiana na hilo zaidi ya
kutoa kauli zenye viashiria vya hali kama hiyo.
Aidha, ilielezwa kuwa Kiiza anaweza kutemwa
pamoja na Mganda mwenzie, Juuko Murshid
kutokana na kufuata mkumbo wa kugoma
kuichezea timu hiyo mpaka wapewe mishahara
yao.
Rais wa Simba, Evans Aveva amesema kuwa sasa
ni rasmi wameshampa Kiiza mkono wa kwaheri na
hakuna tena kilichopo baina yao na zaidi
wamemtakia kila la kheri huko aendako pamoja na
kumshukuru kwa mchango wake mkubwa alioutoa
kwa timu hiyo msimu uliopita.
“Niseme tu kwamba tumemalizana kistaarabu
kabisa na Kiiza na tunamtakia mema, kila la kheri
huko aendako lakini pia kwa kweli tunamshukuru
kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwa Simba
msimu uliopita,” alisema Aveva.
Kiiza aliyewahi kuichezea Yanga anaungana na
wachezaji wengine wa kigeni waliotemwa msimu
huu klabuni hapo; Mkenya, Raphael Kiongera,
Mrundi, Emiry Nimubona na Mganda, Brian
Majwega.

Chapisha Maoni

 
Top