0
Wakati jeshi la polisi likisema linajiimarisha,
vitendo vya ujambazi vinazidi kuitikisa nchi baada
ya kundi la watu wasiojulikana kuvamia ofisi za
Kampuni ya Ahsante Tours ya mjini Moshi, kuua
walinzi wawili na kuiba Sh 65.5milioni.
Tukio hilo limekuja siku chache baada ya watu
wasiojulikana kuvunja duka la kubadilisha fedha
la Chase Forex Bureau De Change la mjini Moshi
na kuiba zaidi ya Sh120 milioni.
Mbali na tukio hilo, Juni 12 mwaka huu, watu
watano wakiwa na bunduki aina ya SMG,
walivamia mji wa Magugu wilayani Babati mkoani
Manyara na kupora Sh2.5 milioni.
Tofauti na tukio hilo la Magugu, hivi karibuni
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam waliwaua
watu watatu eneo la Masaki katika majibizano ya
risasi na Polisi.
Ukiachilia matukio hayo, taarifa kutoka mikoa
mbalimbali nchini zinaonyesha uporaji wa fedha
na mali kwa kutumia pikipiki maarufu kama
bodaboda, unazidi kushika kasi maeneo
mbalimbali.
Wengi wa wanaolengwa na wahalifu hao ni wateja
wanaotoka kuchukua pesa benki au
wanaokwenda kuchukua fedha jambo ambalo
limezua hofu kuwa huenda baadhi ya wafanyakazi
wa benki wanashirikiana na wahalifu.
Lakini, tishio kubwa zaidi la uhalifu linatokana na
kuibuka kwa makundi ya kihalifu yanayokuwa
yamejihami kwa silaha za kivita, yakiwamo
mabomu ya kurushwa kwa mkono, yakichinja raia
na kupora.
Hivi karibuni, Polisi Jijini Dar es Salaam waliwaua
watuhumiwa hatari wawili waliokuwa wamejihami
kwa bunduki na mabomu, wanaotuhumiwa
kuchinja watu nane Jijini Tanga na watatu Jijini
Mwanza
Hali hii ndio imemsukuma Rais John Pombe
Magufuli, kuwaagiza polisi kuhakikisha
‘wanawanyang’anya’ majambazi silaha haraka
kabla ya kuwadhuru polisi ama raia wasio na
hatia.
Uporaji Ahsante Tours
Tukio la mauaji ya walinzi wawili ofisi za Ahsante
Tours, lilitokea usiku wa kuamkia jana, baada ya
watu hao kuwazidi nguvu walinzi na kuwafunga
kamba kisha kuwapiga kwa kitu butu kichwani.
Kampuni hiyo inamilikiwa na mfanyabiashara
Cathbert Swai na mkewe Stella Shangali, ambao
pia wanamiliki hoteli ya kitalii ya Weruweru River
Lodge iliyopo Mailisita, nje kidogo ya mji wa
Moshi.
Taarifa kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi wa
kampuni hiyo ambayo ni moja kati ya kampuni
zinazoongoza kwa kupokea watalii wengi, zinadai
huenda tukio hilo ni mpango wa ndani.
“Kuna maswali mengi tunajiuliza. Walijuaje kuna
kiasi hicho kikubwa cha fedha kama taarifa
hazikutoka miongoni mwetu?” alihoji mmoja wa
wafanyakazi aliyeomba jina lake lisitajwe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad
Mutafungwa, alisema kati ya fedha zilizoibwa,
kulikuwa na Dola za Marekani (Sh50 milioni) na
Sh15 milioni za Tanzania.
Walinzi waliouawa wametajwa kuwa ni Omar
Mohamed (48), mkazi wa Matindigani Pasua na
Dominick Cheddy (41), mkazi wa Mailisita na
wote ni wenyeji wa mkoa wa Tanga.
Kamanda Mutafungwa alisema tukio hilo
liligunduliwa saa 1.00 asubuhi na wasamaria
wema waliotoa taarifa polisi, na uchunguzi wa
awali umebaini watu hao walikata uzio wa ofisi
hizo.
“Baada ya kuingia ndani ya jengo hilo la ofisi
walivunja ofisi ya meneja mkuu na baadaye ofisi
ya mhasibu ndio wakaiba Dola 23,300 na pesa za
Tanzania Sh15 milioni,” alisema Kamanda
Mutafungwa.
“Tunashuku kuwa huenda hao majambazi
waliamua kuwaua hao walinzi baada ya hao
walinzi kuwatambua. Bahati mbaya hawakuwa na
silaha yoyote hata panga hawakuwa
nalo,” alisisitiza.
Kamanda Mutafungwa alisema Polisi inamshikilia
mtu mmoja ambaye inaonekana alikuwepo wakati
mauaji na uporaji huo ukifanyika lakini,
majambazi hao hawakumdhuru sehemu yoyote.
Hata hivyo, Kamanda Mutafungwa, aliwataka
wafanyabiashara kupeleka pesa benki badala ya
kuzihifadhi ndani au ofisini na kuwataka pia
kuimarisha ulinzi ikiwamo kuweka CCCTV
Camera.
Alitoa wito kwa wananchi wenye taarifa za
waliohusika na tukio hilo, kulisaidia Jeshi la Polisi
kama ilivyotokea wiki moja iliyopita ambapo
taarifa zao zilisaidia kuwatia mbaroni wahalifu
mbalimbali 30.

Chapisha Maoni

 
Top