0
WATU 11 wamekufa papo hapo na wengine 44 kujeruhiwa katika ajali mbili tofauti zilizotokea sehemu moja, zikihusisha basi la abiria,
lililopamia malori mawili ya mizigo yaliyogongana uso kwa uso na kuungua moto eneo la Dakawa –
Veta, wilayani Kilosa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ulrich
Matei alisema mjini hapa jana kuwa ajali ya kwanza, malori mawili ya mizigo yaligongana uso kwa uso juzi saa 12 jioni na kuwaka moto.
Katika ajali hiyo ya juzi jioni, lori la mizigo aina
ya Scania ambalo namba za mbele
hazikutambuliwa, lakini tela lake ni namba T 704
CEC, likitoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa, liligongana uso kwa uso na lori aina ya Fuso yenye namba za usajili T 963 BLW,
lililokuwa likitokea Dodoma kwenda Dar es Salaam.
Kamanda Matei alisema katika ajali hiyo, watu watano walipoteza maisha papo hapo kwa kuungua moto mpaka ikashindikana kuwatambua,
akiwemo dereva wa bodaboda aliyekuwa pembeni
mwa barabara na pikipiki yake katika eneo la tukio.
Wengine waliokufa papo hapo na kushindwa
kutambulika kwa mujibu wa Kamanda Matei, ni madereva wa malari hayo na wasaidizi wao
wawili; mmoja kwa kila lori.
Alisema chanzo cha ajali hiyo, ni kutokana na
gari ndogo iliyokuwa mbele ya Fuso hilo
kusimama ghafla na kusababisha dereva wa Fuso
kupita pembeni bila kuangalia mbele na
kugongana uso kwa uso na Scania yenye
shehena ya mafuta na kusababisha malori hayo kuwaka moto.
Wakati malori hayo yakiwa eneo la tukio, jana
alfajiri kulitokea ajali nyingine ambapo basi la abiria mali ya Kampuni ya Otta Classic yenye
namba za usajili T 201 DGK aina ya Higer,
liliparamia moja ya malori yaliyokuwa yamepata
ajali katika eneo hilo na kuua watu sita papo hapo
na kujeruhi wengine 44.
Kamanda Matei alisema kati ya majeruhi hao, sita
hali zao ni mbaya na walikimbizwa katika
Hospitali ya Rufaa ya Morogoro kupatiwa
matibabu zaidi. Alisema ajali hiyo ilitokea saa 10
alfajiri ya Julai Mosi mwaka huu, wakati basi hilo
likitokea Bukoba mkoani Kagera kwenda Dar es
Salaam.
Waliokufa katika ajali hiyo kwa mujibu wa
Kamanda Matei ni dereva wa basi hilo, msaidizi
wake, kondakta na abiria wengine watatu.
Alitaja majina ya waliokufa kuwa ni Yassin
Mgongolwa (41) dereva wa basi hilo, Veronica
Jeremia ambaye ni kondakta, Said Shomari
Simba (30) dereva msaidizi na abiria Lilian Paul
(34), Jonia Kokumbuga na mwamamke mwingine
mwenye umri kati ya miaka 30 -35, ambaye
hajatambulika.
Miili ya marehemu hao na maiti zilizoungua na
kushindwa kutambuliwa, imehifadhiwa katika
chumba cha maiti cha Hospitali ya Rufaa ya
Morogoro.
Kamanda Matei alisema kabla ya basi hilo kupata
ajali, lilisimamishwa na askari wa usalama
barabarani, lakini dereva alikaidi na kupitiliza na
baada ya muda likapata ajali hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe,
ambaye pia alifika eneo la tukio hilo jana, alisema
miili iliyoungua, itatambuliwa kwa kutumia
vinasaba (DNA) na kuwataka ndugu na jamaa zao
kuwa na subira wakati utambuzi huo
utakapofanyika.
Alilipongeza Jeshi la Polisi mkoa na vikosi vya
Zimamoto na wananchi wa vijiji vya karibu na
eneo la ajali kwa kusaidia kuzima moto na
kuokoa majeruhi wa ajali hiyo.

Chapisha Maoni

 
Top