Yanga wakati wanaendelea na zoezi la usajili wapo kwenye mazungumzo na wachezaji wao waliomaliza mkataba Ngoma, Kamusoko, Bossou na Kaseke
Kiungo wa Yanga Deusi Kaseke kesho anatarajia kuongeza mkataba wa miaka miwili baada ya kukamilisha mazungumzo na uongozi wa mabingwa wa Ligi Kuu Bara.
Kaseke ameiambia Goal, yupo njiani leo akielekea Dar es Salaam kwa ajili ya mazungumzo hayo ambayo anaamini yatakuwa na tija ndani yake na yeye kusaini mkataba mpya.
“Nipo njiani nakwenda kuzungumza na viongozi wangu najua hatuwezi kushindwana kwa sababu Yanga ni nyumbani nimefanya kazi pale kwa misimu miwili bila tatizo na mtu,” amesema Kaseke.
Kiungo huyo, ni kati ya wachezaji 13 ambao mikataba yao imemalizika mwishoni mwa msimu uliopita akiwemo Donald Ngoma, Thabani Kamusoko, Vincent Bossou na Haruna Niyonzima anayetarajiwa kumwaga wino wakati wowote Simba.
Awali kiungo huyo ilidaiwa kufuatwa na viongozi wa Singida United kwa ajili ya kumpa mkataba wa kuichezea timu hiyo kwenye msimu ujao wa ligi ya Kuu.
Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa amesema wakati wakiendelea na zoezi la usajili kwa kusajili wachezaji wapya pia wanaendelea na mazungumzo na wachezaji wao ambao walimaliza mikataba yao na mmoja wapo ni Kaseke ambaye kesho wanaweza kufikia muafaka.
Chapisha Maoni
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.