0
Simba ipo katika harakati za kuboresha kikosi chake baada ya kufanikiwa kurejea kwenye michuano ya Afrika, na Bokungu ataonyeshwa mlango wa kutokea
Klabu ya Simba imepanga kuachana na beki Janvier Bokungu kutoka DR Congo baada ya kumrudisha kundini Shomari Kapombe na Ally Shomari anayemudu kucheza nafasi hiyo ya beki wa kulia.
Makamu wa Rais wa klabu hiyo Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ameiambia
Goal, Bokungu alikuwa na mchango mkubwa kwao lakini wanalazimika kuachana naye kutokana na ukubwa wa michuano wanayoelekea kushiriki msimu ujao.
“Bokungu ni mchezaji mzuri na ametusaidia sana msimu uliopita,lakini baada ya kuwapata Kapombe na Ally, tunafikiria kuachana naye kwa sababu hatokuwa na nguvu za kumudu ushindani na vijana,” amesema Kaburu.
Kiongozi huyo amesema kwanza Bokungu alishamaliza mkataba wake hivyo hawaoni haja ya kuendelea kutumia garama kubwa kwa mchezaji kama huyo.
Amesema bado wanajadiliana na kocha kuhusiana na mchezaji huyo na pindi watakapofikia muafaka wataweka wazi kama wataendelea naye au kumshukuru kwa mchango wake.
Simba wanaamini Kapombe na Ally Shomary watatosha sana kwa beki ya kulia, hivyo Bokungu, beki wa zamani wa TP Mazembe ya kwao na Esperance ya Tunisia, ambaye amemaliza mkataba wake anaweza kuruhusiwa kuondoka, ingawa mazungumzo ya mkataba mpya yalikwishaanza.
Simba ipo katika harakati za kuboresha kikosi chake baada ya kufanikiwa kurejea kwenye michuano ya Afrika kufuatia kuikosa kwa miaka mitano.
Simba imekwishasajili wachezaji sita wapya, ambao mbali na Kapombe na Shomari wengine ni kipa Emanuel Elias Mseja, mabeki Jamal Mwambeleko waliosajiliwa kutoka Mbao FC, Yussuf Mlipili kutoka Toto Africans zote za Mwanza na mshambuliaji John Bocco kutoka Azam FC.

Chapisha Maoni

 
Top