Siku ya leo kuna habari mbalimbali zilizoenea mitaani zikimhusisha mchezaji huyo kusaini Simba lakini amekanusha kwa kusema bado hajasaini kokote
Nahodha wa timu ya taifa ya Rwanda, Haruna Niyonzima, bado anaendelea kuumiza vichwa vya mashabiki wa timu za Yanga na Simba wakitaka kujua atasaini timu gani kati ya hizo mbili.
Niyonzima amesema kwa njia ya Mtandao hadi sasa hajasaini timu yoyote kati ya hizo mbili, ingawa amekiri kuwa pande zote mbili zimekuwa zikimfuata kutaka kuzichezea timu zao.
“Hivi karibuni watu watajua ni timu gani nitacheza msimu ujao lakini kwasasa, sijasaini timu yoyote na mkataba wangu na Yanga bado hauja malizika hadi mwishoni mwa mwezi huu hivyo kwa sasa mimi bado ni mali ya Yanga,” amesema Niyonzima.
Kiungo huyo aliyetamba na mabingwa wa soka Tanzania Yanga kwa misimu sita, amesema baada ya kumaliza majuku ya timu yake ya taifa kwasasa anapumzika na familia yake na baada ya muda atakuja nchini kwa ajili ya kukamilisha mazungumzo na timu ambayo ataamua kuichezea.
Amesema amepokea ofa kutoka Simba na timu yake ya Yanga lakini anachofanya kwasasa ni kutuliza akili na kuwashirikisha wanasheria wake ili kuona wapi ni sehemu sahihi kwake kucheza.
Siku ya leo kuna habari mbalimbali zilizoenea mitaani zikimhusisha mchezaji huyo kusaini Simba lakini yeye mwenye amekanusha kwa kusema bado hajasaini timu yoyote kati ya hizo mbili.
Niyonzima ametua Yanga kwa mara ya kwanza mwaka 2011, akitokea APR ya Rwanda na kwa muda wote huo ameweza kuichezea timu hiyo kwa mafanikio makubwa na kubeba mataji mbalimbali ikiwemo ubingwa wa ligi ya Vodacom mara tatu mfululizo.
Chapisha Maoni