SIMBA sasa inataka kuchukua umiliki wa timu ya taifa, Taifa Stars, ambapo kwanza imehakikisha safu yote ya ulinzi ya Stars ikiongozwa na kipa Aishi Manula inahamia Msimbazi kuanzia msimu ujao.
Mnyama anafanya usajili wa nguvu kujiimarisha kwa ajili ya Kombe la Shirikisho mwakani pamoja na kuhakikisha anatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu ujao baada ya kuukosa muda mrefu.
Wakati Yanga bado ikiwa kwenye msoto wa kiuchumi, Simba ilianza na kipa wa Stars, Aishi Manula ambaye atatambulishwa punde baada ya mkataba wake na Azam kufikia ukingoni mwezi ujao.
Manula amesajiliwa Simba sambamba na aliyekuwa nahodha wake, John Bocco.
Manula ambaye ni mshindi mara mbili mfululizo wa tuzo ya Kipa Bora wa Ligi Kuu, anakuwa mchezaji wa kwanza katika safu hiyo ya ulinzi ya Stars na usajili wake huenda utamchomoa Msimbazi, kipa Mghana, Daniel Agyei.
Simba wana mtuhumu Agyei kwamba alicheza chini ya kiwango ili Simba iondolewe kwenye michuano ya SportPesa awahi harusi ya mwenzake, James Kotei.
Taarifa ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba Simba ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wa beki wa kati wa Stars, Salim
Mbonde ambaye mkataba wake na Mtibwa Sugar umefikia ukingoni.
Mbonde amekuwa tegemeo sasa katika kikosi cha Stars hasa baada ya wakongwe, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondan kutundika daluga
kuichezea timu ya Taifa huku beki mwingine wa kati, Aggrey Morris akiondolewa Stars baada ya Zanzibar kupata uanachama wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Mbonde anakuwa akicheza katika beki ya kati sambamba na kiraka wa Simba, Abdi Banda ambaye hata hivyo huenda akatimkia nchini Afrika Kusini.
Hata hivyo beki huyo huenda pia akaongeza mkataba Simba baada ya bilionea, Mohammed Dewji ‘MO’ kuingia kati usajili wake.
Wakati huo huo beki ya kushoto ya Stars sasa ipo chini ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye ni beki tegemeo pia wa Simba. Tshabalala hatacheza mechi ya leo dhidi ya Lesotho kutokana na kusumbuliwa na majeraha lakini ndiye mwenye nafasi hiyo.
Beki mwingine wa kushoto, Haji Mwinyi aliyekuwa akimpa Tshabalala upinzani naye ameondolewa Stars kwani atakuwa akiichezea timu ya taifa ya Zanzibar ambayo imekuwa mwanachama wa CAF.
Simba pia ipo katika mazungumzo ya mwisho na beki wa kulia wa Azam, Shomary Kapombe ambapo muda wowote anaweza kusaini, itakuwa ni hitimisho la safu yote ya ulinzi ya Taifa Stars kuhamia Simba.
Kapombe ameahidiwa mambo mazuri na vigogo wa Msimbazi ambao wamekubaliana na dau lake pamoja na mshahara.
Lakini bado hajamwaga wino rasmi, ingawa Simba wamesisitiza kwamba hawana presha naye.
Staa mwingine wa timu ya Taifa ya Uganda, Emmanuel Okwi atasaini mkataba wikiendi hii.
Hayo yote yanafanyika ili kuhakikisha Simba inakuwa na makali ya kutosha msimu ujao kuweza kutwaa taji la Ligi Kuu Bara pamoja na kuifanya vizuri anga la kimataifa katika Kombe la Shirikisho.
Chapisha Maoni
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.