Tanzania 'Taifa Stars' itaanza harakati zake za kusaka kufuzu kwa fainali za Mataifa Afrika 2019, kesho Jumamosi kwa kuikabili Lesotho kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi saa 2:00 usiku.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), litangaza viingilio vya mchezo huo kuwa ni Sh
Sh 10,000 kwa Jukwaa Kuu wakati mzunguko itakuwa ni Sh 5,000.
Tanzania ipo Kundi L pamoja na Uganda, Cape Verde na Lesotho ambako kinara wa kundi hilo anakata tiketi ya moja kwa moja kwenda Cameroon.
Kocha wa Stars, Salum Mayanga itakuwa ni mechi yake ya kwanza ya mashindano tangu alipochukua jukumu hilo kutoka kwa Boniface Mkwasa.
Katika mchezo huo kwa mara ya kwanza Stars tangu muungano Tanyangika na Zanzibar 1965, itacheza bila ya wachezaji kutoka visiwani kutokana na kupewa uachama wa CAF.
Kocha Mayanga anajua ushindi katika mchezo huo utamuongezea kujiamini pamoja na kuvuta mashabiki wengi wa Stars ambao wamepoteza matumaini kutokana na mwenendo wa kusuasua wa timu hiyo.
"Maandalizi yamekamilika kwa asilimia kubwa, tulikuwa kambini nchini Misri tumerejea na dhamira yetu ni kuhakikisha kwa njia yoyote tunaibuka na ushindi na uwezo huo," alisema Mayanga.
Tanzania mara ya mwisho kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika ilikuwa 1980.
Nahodha Mbwana Samatta anayechezea Genk ya Ubelgiji, Farid Musa wa Tennerife ya Hispania pamoja na Thomas Ulimwengu (AFC Elkistuna) wanatazamwa kama watu pekee wanaoweza kutimiza kwa 100% jukumu hilo la kufunga mabao na kuendeleza rekodi nzuri ya kocha Salum Mayanga ambaye hajapoteza mchezo wowote tangu alipoanza kuinoa timu hiyo.
Chini ya Mayanga, Stars imeibuka na ushindi kwenye mechi mbili za kirafiki dhidi ya Botswana ambayo ilishinda mabao 2-0 na ile dhidi ya Burundi ambayo iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Mabadiliko kadhaa yanatarajiwa kufanywa kwenye kikosi cha Stars ambapo Ulimwengu na Gadiel Michael wana nafasi kubwa ya kuanza wakichukua nafasi za Mohammed Hussein 'Tshabalala ' aliye majeruhi sambamba na Ibrahim Ajibu.
Faida kubwa kwa Stars kwenye mchezo wa leo ni uwepo wa kundi kubwa la washambuliaji wenye uwezo wa kucheka na nyavu ambapo ukiondoa Samatta, Farid na Ulimwengu bado kuna Saimon Msuva na Abdulrahman Mussa walioibuka wafungaji bora wa ligi kuu msimu uliomalizika pamoja na Mbaraka Yusuph aliyewafuatia.
"Maandalizi yetu yamekamilika ambapo mbali ya programu za kiufundi, tumefanikiwa kutazama mechi zao mbili kupitia mikanda ya video ambapo tumefanikiwa kubaini ubora na udhaifu wao.
Timu iko imara na tutamkosa Mohammed Hussein tu kati ya wale tuliosafiri nao kule Misri ambaye ni majeruhi lakini wengine wote ni wazima. Tulichokipanga kama timu ni kutumia vizuri uwanja wa nyumbani ili kupata matokeo mazuri.
Tunachoomba ni Watanzania wote kuwa pamoja na timu kwani inawasaidia wachezaji kuhamasika na kupambana kwa dakika zote 90 ili kusaka ushindi," alisema Mayanga.
Kocha wa Lesotho, Moses Maliehe alisema kuwa pamoja na timu yake kutokuwa na nyota wengi wanaocheza nje, matumaini yao ni kupata matokeo yatakayoishtua Stars.
"Hili ni kundi ambalo liko wazi kwa kila timu hivyo kutegemeana na jinsi itakavyochanga karata zake. Tunajua Tanzania ina baadhi ya wachezaji wanaocheza nje ya nchi ambao bila shaka watakuwa tishio lakini tutawadhibiti.
Sisi tuna wachezaji wawili wanaocheza soka la kulipwa nje ya Lesotho ambao naamini wataiongoza vyema timu kupata matokeo mazuri ugenini, " alisema Maliehe.
Chapisha Maoni