DIRISHA la usajili limefungwa juzi Alhamisi saa sita usiku huku timu zikifanya usajili kulingana na mahitaji yao, usajili ambao zinaamini utazisaidia kuleta ushindani msimu ujao wa Ligi Kuu.
Katika usajili huo, timu nyingi zimeongeza wachezaji katika kila nafasi ili kuhakikisha hata anapokosekana mmojawapo, basi kunakuwa na mbadala wake ambaye ataziba pengo hilo vizuri.
Mwanaspoti limeangalia usajili wa baadhi ya klabu na kuona kutakuwa na bato kubwa la wachezaji kwa wachezaji katika kuhakikisha wanagombania namba ili kupata nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza.
KANGWA vs MWASAPILI
Hakuna ambaye hajui uwezo wa Bruce Kangwa msimu uliopita kacheza takribani mechi zote, katika mechi 30 alikosa mchezo mmoja baada ya kupata kadi iliyomfanya akae nje.
Uwezo wake wa kupanda kupiga krosi na kushuka kwa kasi kukaba, kila kocha anavutiwa nao. Hali iliyomfanya kuwa mchezaji pekee aliyecheza mechi mfululizo ndani ya Azam FC.
Baada ya kutua Hans Pluijm ameamua kumsajili Hassan Mwasapili ili kuongeza changamoto kwa Kangwa lakini bado kutakuwa na upinzani mkali kati yao kwani Kangwa sio rahisi kukaa nje kizembe.
Mwasapili alikuwa nahodha na mchezaji wa panga pangua upande wa kushoto Mbeya City, lakini anaenda kukutana na changamoto kutoka kwa Kangwa ambaye tangu atueAzam amekuwa na misimu bora mfululizo.
HASSAN DILUNGA vs SAID NDEMLA
Kwanza kabisa mashabiki wa Simba wanataka kuona kama Hassani Dilunga atafanya vizuri akiwa na kikosi hicho kama ambavyo alifanya akiwa na Mtibwa Sugar.
Wakati huo huo mashabiki walikuwa hawakubaliani na viongozi wa Simba kuona Said Ndemla anaondoka kizembe klabuni hapo, hivyo waliwataka wamalizane nae mapema ili abaki kikosini.
Wote kwa pamoja wamekutana kitu kikubwa ni viungo hawa kuwa na uwezo mkubwa wa kuchezea mpira hivyo aina ya soka la utulivu pale Simba litakuwa linachezeka vizuri na kwa utulivu.
Ndemla, msimu uliopita alikuwa hapati nafasi ya kucheza katika kikosi cha Pierre Lechantre, kwa sababu kocha huyo alitaka soka la kukaba sana hali iliyomfanya akalie benchi.
Masoud Djuma na Patrick Aussems wote ni wachezaji wanaopenda soka la chini, hivyo wachezaji hawa watakuwa na kazi kubwa ya kupambana kupata namba ya kuanza kwani wote wana soka la aina moja.
MUDATHIRI YAHYA vs SALMIN HOZA
Mudathir Yahya alikuwa na kiwango kizuri akiwa na kikosi cha Singida United. Timu kadhaa zilihitaji huduma yake kutokana na aina yake ya kukaba na kupiga pasi fupi na ndefu.
Ametua Azam FC na katika mechi za Kombe la Kagame amekuwa akichezeshwa mfululizo baada ya kuwa Salum Aboubacary, Frank Domayo na yeye huku wakielewana vya kutosha.
Katika kikosi hicho kuna nyota mwingine Salmin Hoza, alikuwa na msimu mzuri na uwezo wake wa kukaba na kupiga pasi pamoja na mashuti yake yaliyoshiba. Kocha Hans Pluijm anaweza kuwa katika wakati mgumu kupanga kikosi chake.
Kwa namna moja au nyingine uwezo wa wachezaji hawa utakuwa na faida kwa Azam FC kwani kikosi chake kinazidi kuwa kipana, pia hata kama mmoja anapokosekana, basi anayeingia anakuwa bora zaidi.
ABDALLAH KHERI vs YAKUB MOHAMMED
Ukuta wa Azam FC ni kati ya kuta ambazo zimeonekana kukomaa vilivyo. Aggrey Morris amekuwa kiongozi mzuri katika safu ya ulinzi ya Azam.
Ujio wa Yakub Mohammed uliongeza tija kwani ukuta ulizidi kuwa mgumu na utulivu wa mchezaji huyo uliwafanya mashabiki wengi kuvutiwa na aina yake ya uchezaji.
Yakub alipata majeraha na kushindwa kumalizia mechi za ligi, nafasi yake ilichukuliwa na Abdallah Kheri ‘Sebo’ ambaye tangu amepata nafasi hiyo ameonyesha ukomavu wa hali ya juu.
Sebo katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagame alikuwa ni miongoni mwa mabeki wanaofanya vizuri lakini kurejea kwa Yakub ambaye alikuwa anasumbuliwa na majeraha kutakuwa na changamoto kwa upande wake kutokana na beki huyo pia kujitengenezea ufalme wake ndani ya Azam.
AISH MANULA vs DEOGRATIUS MUNISH ‘DIDA’
Hili ni bato la aina yake katika kikosi cha Simba kwa sababu makipa hawa wote kwa nyakati tofauti waliwahi kuwa namba moja kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania.
Dida ni miongoni mwa makipa wenye kiwango kizuri akiwa na kikosi cha Yanga kabla hajatimkia katika timu ya Pretoria University (Turks) Afrika Kusini inayoshiriki Ligi Daraja la kwanza.
Usibishe katika hilo kwani mchezo wa mwisho Simba dhidi ya Kagera, golini alikaa Said Mohammed ‘Nduda’ na mshambuliaji wa Kagera Sugar, Edward Christopher ndiye alitibua shughuli hiyo kwani bao lake liliwalaza chali Simba na kutibua rekodi hiyo.
Ushindani wa namba uliopo kati ya Manula na Dida ni mkali sana, lakini kocha ndiye mwenye uamuzi ya mwisho nani akae kwenye lango la Simba.
JOHN BOCCO vs MEDDIE KAGERE
Ujio wa Kagere na uwezo wake aliounyesha akiwa na kikosi cha Simba kwenye michuano ya Kombe la Kagame bila shaka hakuna mtu ambaye anahoji uwezo wake alionao mchezaji huyu.
Lakini ikumbukwe kwamba nafasi ambayo anacheza kuna nahodha John Bocco ambaye hakucheza michuano hiyo na watakutana kwenye Ligi Kuu.
Kwa wachezaji hawa kutakuwa na bato kubwa hapo baadaye kwa sababu wote wawili wana uwezo mkubwa lakini ni ngumu Bocco kuanzia nje kwa sababu ni nahodha, Kagere akifanya vizuri ana uwezo mkubwa wa kupindua meza.
Bocco anatakiwa kuongeza juhudi na kutupia mabao kadiri anavyoweza ili kulishawishi benchi la ufundi hasa kocha mpya Aussems ambaye amemuona Kagere akicheza mechi na siyo Bocco.
DITRAM NCHIMBI vs DONALD NGOMA
Kwa maumbo wote ni wachezaji ambao wana maumbo mazuri ya kucheza nafasi ya ushambuliaji.
Nchimbi alitakata akiwa na kikosi cha Mbeya City mpaka Njombe Mji na kuwafanya mabosi wa Azam FC kuvunja vibubu kumsajili.
Nchimbi amesajiliwa na Azam akiwa ametoka katika timu ambayo haikuwa na muunganiko mzuri lakini alionyesha kiwango kikubwa na kufanya klabu nyingi kuvutiwa na huduma yake ikiwemo Mbeya City waliotaka kumrudisha kikosini.
Azam haikuishia hapo ilizama mfukoni na kumchukua Donald Ngoma ambaye alikuwa nje ya uwanja kutokana na kusumbuliwa na majeraha.
Ngoma kama akiwa fiti asilimia 80 kwa vyovyote kutakuwa na kazi nzito katika nafasi hiyo kwa sababu Ngoma anasubiriwa na wengi kuona namna ambavyo anavyoweza kucheza baada ya kukosekana kwa muda mrefu huku Nchimbi akitaka kupambana zaidi na kuonyesha kuwa Azam hawakufanya makosa kumsajili.
HARUN CHANONGO vs SALUM KIHIMBWA
Msimu uliomalizika Salum Kihimbwa ndiye aliyekuwa nyota katika kikosi hicho cha Mtibwa Sugar. Uwezo wake wa kukimbia na mpira pamoja na kuuchezea ulikuwa unawavutia mashabiki wengi.
Uwezo wake ulimfanya Harun Chanongo awe chaguo la pili katika kikosi hicho, lakini msimu ujao kutakuwa na kazi kubwa kwa wachezaji hawa wawili kwani Chanongo hatataka kuendelea kuwa mchezaji wa akiba.
Kihimbwa naye anataka kuonyesha makali yake ya mwisho kwani amebakiza mkataba wa mwaka mmoja, hivyo atataka kuonyesha makali yake ili kupata timu ya maana dirisha dogo au msimu ukimalizika.
Chapisha Maoni
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.