MSIMAMO WA MH. ZITTO KABWE KUHUSU MCHAKATO WA KUANDIKA KATIBA MPYA
Jana tarehe 29 Julai, 2014 nimefanya
mahojiano katika kipindi cha
PowerBreakFast kinachorushwa na
Clouds FM. Baadhi ya vyombo vya
habari vimeandika mahojiano yale.
Napenda nitoe ufafanuzi kidogo kuhusu
msimamo wangu kuhusu mchakato wa
Katiba.
Kwanza, Mimi sijawahi kuwa UKAWA
wala kundi lolote lile katika Bunge
Maalumu la Katiba isipokuwa kundi
linalotaka maridhiano. Msimamo wangu
kuhusu Muungano ni Serikali Tatu
Zilizoboreshwa (S3z) ili kuwa na
Muungano imara usio tegemezi wala
egemezi kwa Washirika wake.
Pili, Mimi niliunga mkono ‘protest’ ya
baadhi ya Wajumbe wa Bunge Maalumu
la Katiba kupinga lugha za matusi na
lugha za kibaguzi zilizokuwa
zinaendelea ndani ya mkutano ule.
Vilevile niliunga mkono kwamba Rasimu
inayopaswa kujadiliwa ni Rasimu
iliyotokana na Tume ya Marekebisho ya
Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Sinde
Warioba. Nasisitiza umuhimu wa kupata
Katiba BORA itakayoimarisha DOLA ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tatu, kwa hali ya sasa kuna mkwamo
katika kupatikana kwa Katiba Bora.
Mkwamo unaotokana na kutokuwepo
kwa nia ya dhati ya kupata maridhiano
ya pande zinazopingana. UKAWA
hawataki mazungumzo na Viongozi wa
Bunge la Katiba badala ya kujenga
maridhiano kila siku wanawabeza
UKAWA jambo ambalo kamwe haliwezi
kujenga mwafaka. Ushauri wangu ni
kuahirisha mchakato mzima wa
kuandika Katiba mpaka mwaka 2016
baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2015. Katiba ya sasa ifanyiwe
marekebisho machache kama ifuatavyo;
i) Tume ya Uchaguzi ili iwe huru na
ionekane kuwa huru, ikiwemo
kuwaondoa watumishi wa Halmashauri
za Wilaya, Miji na Majiji katika
kusimamia uchaguzi
ii) Kuruhusu mgombea binafsi
iii) Kuondoa Mafuta na Gesi kama
Jambo la Muungano ili Zanzibar ianze
mara moja kusimamia kwa uhuru
utafutaji wa Mafuta katika vitalu
vilivyopo upande huo wa Muungano
Mkutano wa Bunge Maalumu
utakaofanyika bila kuwepo kwa
maridhiano utakuwa hauna maana
yeyote na itakuwa ni sawa na kupoteza
muda na fedha za walipa kodi ambazo
zingeweza kununua madawa vijijini.
Mimi binafsi sitahudhuria mkutano wa
Bunge Maalumu kama makundi hasimu
hayatakuwa yamefikia maridhiano.
Kabwe Zitto,
MB/MBMK
Chapisha Maoni